RAMADHAN HASSAN -DODOMA
KIFO cha Mwanadiplomasia mahiri na mwanausalama nchini, Balozi Augustine Mahiga kimeshtua na kuliza wengi ndani na nje ya nchi.
Taarifa za Dk. Mahiga ambaye kwa sasa alikuwa Waziri wa Katiba na Sheria na hapo kabla Waziri wa Mambo ya Nje katika serikali ya awamu ya tano kufariki dunia zilitangazwa mapema jana asubuhi na Rais Dk. John Magufuli kupitia taarifa iliyotolewa na Kurugenzi ya Mawasiliano Ikulu.
Umoja wa Mataifa, Balozi za Canada, Sweden, Ufaransa, China na baadhi ya viongozi mbalimbali ndani na nje ya Tanzania wametoa salamu wakimlilia Balozi Mahiga.
Wanasiasa wakiwamo wa wale wa upinzani nao wameonekana kumzungumzia vizuri Balozi Mahiga na wengine wakienda mbali na kumwelezea kwamba alikuwa ni tofauti na wabunge wengine wa CCM hali kadhalika mawaziri.
Balozi Mahiga mbali na kuwa sifa ya mwanadiplomasia mahiri aliyefanya kazi za kimataifa kwa miaka mingi pia amelitumikia taifa katika nafasi nyingine nyingi nyeti ikiwamo ile ya Ukurugenzi wa Usalama wa Taifa.
Balozi Mahiga amepewa heshima hiyo si tu kwa sababu umahiri wake katika eneo la diplomasia au uzoefu mkubwa na nafasi nyeti alizowahi kushika ndani na nje ya Tanzania, bali kile kilichotajwa na wengi, unyenyekevu na kutopenda kujikweza .
Hilo limeonekana wazi katika ujumbe uliotumwa kwenye mitandao mbalimbali ya jamii si tu na wanasiasa bali na makundi mbalimbli ya watu, wakiwamo wale waliozungumza na gazeti hili.
Hata Rais Magufuli mwenyewe amethibitisha hilo kupitia taarifa ya Ikulu.
“Pamoja na umri wake mkubwa na uzoefu wa kushika madaraka katika nyadhifa mbalimbali za Kitaifa na Kimataifa, marehemu Balozi Mahiga alikuwa mnyenyekevu na mtiifu kwa kila jukumu nilomtuma,” ameeleza Rais Magufuli katika salamu zake za rambirambi.
Balozi Mahiga ambaye amelitumikia Taifa kwa takribani miaka 45 anakuwa mbunge wa tisa kufariki kwa kipindi cha miaka mitano tangu kuanza kwa Bunge la 11 na mbunge wa tatu ndani ya siku 11.
Wengine waliofariki ni Mbunge wa Viti Maalum (CCM), Dk. Getrude Rwakatare, Mbunge Sumve,Richard Ndassa (CCM).
Waliofariki hapo kabla ni Mbunge wa Newala Vijijini (CCM), Rashid Akbar, Mbunge wa Korogwe Vijijini (CCM), Stephen Ngonyani maarufu kama Profesa Majimarefu, Mbunge wa Viti Maalum (Chadema),Dk. Elly Macha, Mbunge wa Dimani (CCM), Hafidh Ally Tahir, Mbunge wa Songea Mjini (CCM), Leonidas Gama na Mbunge wa Buyungu, Kasuku Bilago.
Kwa mujibu wa taarifa iliyotolewa na Kurugenzi ya Mawasiliano ya Rais Ikulu na kusainiwa na Mkurugenzi wake, Gerson Msigwa, Dk. Mahiga alifariki jana asubuhi nyumbani kwake Jijini Dodoma.
Taarifa hiyo ilieleza marehemu Mahiga alifikishwa Hospitali akiwa tayari ameishafariki dunia.
Katika taarifa hiyo, Rais Dk. Magufuli alitoa pole kwa familia ya marehemu ,Spika wa Bunge Jon Ndugai,Wafanyakazi wa Wizara ya Sheria na Katiba, na wananchi wa Mkoa wa Iringa kwa kuondokewa na mpendwa wao.
Rais,Dk Magufuli alisema anaungana nao katika kipindi hiki kigumu ambapo amemuelezea marehemu kwamba alikuwa ni mchapakazi, mwadilifu, mzalendo, mwanadiplomasia mahiri aliyeiwakilisha na kuipigania Tanzania katika janja za kimataifa kwa miaka mingi.
Umoja wa Mataifa nchini nao umeguswa na kifo cha Balozi Mahiga.
Kupitia andiko lao la kwenye twitter, Umoja huo wa Mataifa umeandika ukisema kuwa unaungana na Taifa kuomboleza kifo cha Balozi Mahiga ambaye alikuwa rafiki wa umoja huo hapa nchini na duniani akiwa amehudumu kama mwakilishi maalumu wa Katibu Mkuu wa umoja huo nchini Somalia.
WANASIASA WA UPINZANI
Kiongozi wa Chama cha ACT-Wazalendo, Zitto Kabwe ameandika kuwa tangu aingie kwa mara ya kwanza bungeni miongoni mwa marafiki wazee aliokuwa nao kwa ajili ya ushauri na masuala mbalimbali ya nchi ni Balozi Mahiga.
Alisema Balozi huyo alikuwa akitaka kuelewa jambo atamuita na kunywa pamoja kahawa.
“Kama kulikuwa na Mtanzania mmoja anayeijua Dunia kwa jicho la usalama (strategic security studies) alikuwa ni Mzee Mahiga, Kanali wa Jeshi, Mkuu wa Usalama wa Taifa na Mwanadiplomasia mbobezi. Pole sana familia, pole sana wabunge,”aliandika Zitto.
Kwa upande wake mbunge wa Chadema katika jimbo la Tarime vijijini, John Heche naye aliandika;
“Leo Taifa limepoteza mtu mwema mbobezi diplomasia, rafiki yangu na baba yangu Mzee Mahiga nakulilia sana, tulikuwa wote bungeni tofauti na wabunge na mawaziri wengi wa CCM ulitambua hotuba yetu ukasifu uwezo na ushauri wa waziri kivuli Salome Makamba. Nitakukumbuka daima”.
Mbunge wa Kawe (Chadema) Halima Mdee naye ameandika;
“Upumzike kwa amani Balozi Mahiga, ulikuwa mtu mwema sana, pole sana kwa familia, Covid -19 ipo na inaua kwa kasi”.
Mbali na wabunge hao wa upinzani ambao ujumbe wao umeonekana kumsifu Balozi Mahiga kwa wema, miongoni mwa wakosoaji wakubwa kwenye mitandao ya kijamii, Maria Sarungi naye ameonekana kumwelezea vyema kiongozi huyo.
“Upumzike wa amani Balozi Mahiga, ulikuwa bora Tanzania na Afrika, ulifanya kazi bila kuchoka, ulikimbia mbio nzuri na kupambana, Pumzika baba”.
Aidha mawaziri wenzake wakiwamo wale vijana nao wamemlilia Balozi Mahiga kama ilivyo kwa wapinzani nao wamemuelezea vizuri.
Waziri wa Uwekezaji Angellah Kairuki ameandika; “Pumzika kwa amani Mh. Mahiga tutakumbuka busara zako, maarifa yako, uzoefu na weledi mkubwa uliokuwa nao baba yetu Mwenyezi Mungu ailaze roho yako mahala pema.
Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto Ummy Mwalimu amemuelezea Balozi Mahiga kama mtu aliyekuwa na roho nzuri.
“A good heart has stop beating! My heartfelt condolences to his family. (moyo mzuri umesimama kupumua, salamu zangu za pole za moyoni kwa familia yake) Mungu awape nguvu katika kipindi hiki kigumu. RIP Balozi Augustine Mahiga, ulikuwa mwema licha ya nafasi kubwa/nyeti ulizowahi kushika nchini na kimataifa”.
Dunia
KIBAJAJI NA UNYENYEKEVU
Mbunge wa Mtera, Livingstone Kibajaji (CCM) amesema atamkumbuka Balozi Mahiga kama mwanadiplomasia nguli ambaye aliitangaza nchi ndani na nje.
“Mimi nilikuwa namwita mjomba na tulikuwa tunaitana mjomba kwa sababu yeye ni Mhehe mimi ni Mgogo, Wahehe na Wagogo ni wajomba, Mahiga namfahamu kama mwanadiplomasia nguli namfahamu kama ni mbobezi katika masuala ya ulinzi na diplomasia,”alisema Mbunge huyo ambaye ni maarufu kwa jina la Kibabaji.
Alisema marehemu alikuwa ni mtulivu na mnyenyekevu ambapo pia alikuwa akimheshimu kila mmoja bila kujali kama ana kitu ama hana.
“Lakini ndani ya Bunge nilijifun
za kitu, alikuwa Waziri wa Mambo ya Nje ni mtu mtulivu mtu mnyenyekevu lakini alikuwa anamweshimu mtu yoyote huwezi kukuta akijimwambafay”
“Ni mtu mcheshi wiki moja tulikutana nae pale Bank ya Bunge akanambia mjomba tupo,kama unamatatizo ya kisheria njoo mjomba alikuwa ni muungwana aliyekuwa akitufundisha unyeyekevu,”alisema.
Naye,Naibu Waziri wa Kilimo,Omari Mgumba alisema amempoteza mtu muhimu ambaye alikuwa msaada mkubwa katika Baraza la Mawaziri kwani alikuwa akitoa ushauri ambao wengi walikuwa wakijifunza kutoka kwake.
“Kwanza tumesikitika sana kumpoteza mzee wetu ambaye sisi kwetu ni kama mwalimu na mimi ndio mara ya kwanza kuingia kwenye Baraza la Mawaziri.
“Tulikuwa tuna mengi ya kujifunza kutoka kwake moja ni uzalendo wake,uchapa kazi wake na alidhihirisha kwamba umri sio tatizo,”alisema Mgumba.
Alisema licha ya kwamba alikuwa na umri mkubwa lakini alikuwa akifanya kazi kama kijana ambaye ndiyo anaanza kazi.
Msemaji Mkuu wa Kambi Rasmi ya Upinzani Bungeni,katika Wizara ya Sheria na Katiba Salome Makamba (Chadema) alisema licha ya maoni ya Kambi hiyo kutokusomwa bungeni wakati wa uwasilishaji wa bajeti ya Wizara hiyo kutokana na kukataliwa lakini watamkumbuka Balozi Mahiga kwani alimfuata na kumwambia kwamba hakulala alikuwa akisoma maoni yao.
“Na juzi wakati tunahitimisha bajeti yetu ya Katiba na Sheria pamoja na kwamba maoni ya kambi yetu yalitupiliwa mbali lakini aliniita aliongea na mimi akasema hakulala usiku kucha alikuwa akisoma hotuba yangu ambayo nilitakiwa kuiwasilisha kesho yake.
“Na akasema nimejibu swali kubwa sana ambalo Wabunge walikuwa wakijiuliza wapinzani wanapodai tume huru ya uchaguzi wanataka nini na nimetumia uwezo wangu wote kulijibu swali hilo.
Alisema marehemu Mahiga alimwambia kwamba licha ya kwamba hotuba hiyo kutosomwa lakini ataitunza na itatumika kama moja ya taarifa muhimu pale ambapo yatajadiliwa mambo ya tume huru ya uchaguzi.
Mbunge huyo wa Viti Maalum alisema anaamini yeyote ambaye atapewa nafasi ya kushika nafasi hiyo atafanya kazi vizuri na wao.
Kwa upande wake Mbunge wa Ulanga Goodluck Mlinga (CCM) alisema vijana watajifunza uadilifu kutoka kwa Balozi Mahiga.
WAUZA MAGAZETI WAMLILIA
Wakizungumza na MTANZANIA jana wauza magazeti katika kijiwe cha jirani na Makao Makuu ya Chama cha Mapinduzi (CCM) walisema watamkumbuka Balozi Mahiga kwa upendo wake kwani alikuwa mteja wao mkubwa wa magazeti yote ya siku husika.
Dora Chisomeko alisema marehemu Mahiga kila siku kabla ya saa tatu asubuhi alikuwa akifika katika kijiwe chake kwa ajili ya kununua magazeti ya siku husika.
“Sijamuona Jumatano na Alhamisi lakini kila siku alikuwa anakuja hapa nampa magazeti mwanzo nilikuwa sijui kama ni Waziri lakini baadae alipokuwa akija na gari lenye namba za Waziri ndio nikagundua kwamba ni Waziri,ni mtu mzuri sana anaupendo wa dhati,”alisema.