25.4 C
Dar es Salaam
Saturday, November 16, 2024

Contact us: [email protected]

Droo ya robo fainali: Hatima ya Simba kujulikana leo

MOHAMED KASSARA-DAR ES SALAAM

BAADA ya kutinga Robo Fainali ya Ligi ya Mabingwa Afrika kibabe kwa kuichapa AS Vita mabao 2-1, Simba leo itajua itavaana na nani katika hatua hiyo.


Saa chache kutoka sasa, droo ya robo fainali itapangwa, ambapo Simba itajua inavaana na nani kati ya vigogo watatu wa soka la Afrika ambao ni TP Mazembe ya Jamhuri ya Kidemokrasia Kongo (DRC), Wydad Casablanca ya Morocco au mabingwa watetezi wa michuano hiyo, Esperance ya Tunisia.


Simba ilimaliza nafasi ya pili kwenye msimamo wa kundi D, nyuma ya Al Ahly ya Misri, hivyo kwa mujibu wa Shirikisho la Soka Afrika (CAF), Wekundu hao wa Msimbazi watakutana na moja ya timu hizo zilizoongoza makundi ya A, B na C.


Kanuni za michuano hiyo zinaeleza wazi kuwa timu zote zilizomaliza nafasi ya pili zitawekwa katika chungu kimoja na zile zilizomaliza kinara zikiwekwa pia chungu kimoja.


Kwa maana hiyo, Simba itakutana na moja kati ya timu kutoka Uarabuni, ambako kuna timu mbili za Wydad Casablanca na Esperance au DRC kuumana na TP Mazembe.


Wydad Casablanca ilimaliza kinara wa kundi A, ikiwa na pointi 10 baada ya michezo sita, Esperance ilimaliza kinara wa kundi B, na pointi zake 14, huku TP Mazembe ikiwa mbabe wa kundi C ikiwa na pointi 11.


Katika hatua hiyo ya robo fainali, Simba itaanzia nyumbani baada ya kumaliza nafasi ya pili, hivyo kinara wa kundi atapata faida ya kuanzia ugenini.
Simba itaanzia kwenye uwanja wa nyumbani, ambapo imekuwa ikifanya vizuri kwa michezo yote dhidi ya wapinzani wao hatua ya kwanza na 16 bora.


Timu hiyo ilianzia hatua ya awali ya michuano hiyo kwa kuvaana na Mbabane Swallows ya Eswatini, huku Simba wakianzia kwenye uwanja wa nyumbani na kufanikiwa kuibuka na ushindi wa mabao 4-1.
Wekundu hao wa Msimbazi waliendeleza rekodi zao nzuri nyumbani katika mchezo wa marudiano wa raundi ya kwanza ya michuano dhidi ya Nkana Red Devils na kushinda kwa mabao 3-1 na kutinga hatua ya makundi.


Katika hatua ya makundi, Simba ilikuwa miongoni mwa timu zilizonufaika na matumizi mazuri ya uwanja wa nyumbani kwa kuvuna pointi tisa, zilizowapeleka robo fainali ya michuano hiyo.
Katika hatua hiyo, Simba ilianza kwa kuicharaza JS Saoura mabao 3-0, ikaichapa Al Ahly bao 1-0, kabla ya kufunga hesabu kwa kuiondoa AS Vita kwa mabao 2-1.

Kuelekea hatua hiyo ya robo fainali, Mtanzania linakuletea takwimu za timu hizo tatu ambazo moja kati hizo itakutana na Simba.

Wydad Casablanca
Timu hiyo ndio mabingwa watetezi wa Kombe la Shirikisho Afrika walilolitwaa msimu uliopita baada ya kuilaza AS Vita kwa jumla ya mabao 4-3 katika michezo miwili ya fainali iliyochezwa nyumbani na ugenini.


Wydad ilianza kwa kuchapwa mabao 3-1 katika fainali ya kwanza iliyochezwa jijini Kinshasa, kabla ya kupindua meza kwa kushinda mabao 3-0 nyumbani na kutawazwa kuwa mabingwa wa michuano hiyo.


Wababe hao wa Morocco walianzia raundi ya kwanza ya michuano hii kwa kuvaana na Jaaraf ya Senegal, ambapo ilianza kushinda mabao 2-0 nyumbani, kabla ya kupoteza mchezo wa marudiano ugenini kwa mabao 3-1, lakini ilitinga hatua ya makundi kutokana na faida ya bao la ugenini.


Timu hiyo ilipangwa kundi A pamoja na timu za Mamelodi Sundown ya Afrika Kusini, ASEC Mimosa ya Ivory Coast na Lobi Stars ya Nigeria.


Wydad ilizindua kampeni zake za hatua ya makundi kwa kuvaana na ASEC na kushinda kwa mabao 5-2 nyumbani, ikichapwa mabao 2-1 na Mamelodi ugenini katika mchezo wa pili, ikaifunga Lobi Stars bao 1-0 nyumbani, kabla ya kulazimishwa suluhu na Lobi Stars katika mchezo wa marudiano.


Ikakubali kichapo cha mabao 2-0 na ASEC ugenini, kabla ya kumaliza hatua ya makundi kwa ushindi wa bao 1-0 dhidi ya Mamelodi bao 1-0 nyumbani.
Katika michezo yake nane ya michuano hiyo, timu hiyo haijashinda mchezo ugenini katika mechi zake nne, imepoteza tatu na kutoka sare moja, ambapo hadi sasa imefunga mabao 10 na kufungwa mabao nane.

ESPERANCE
Timu hiyo ndio mabingwa watetezi wa michuano hiyo ambayo waliitwa msimu uliopita baada ya kuichapa Al Ahly ya Misri katika michezo ya fainali ya nyumbani na ugenini.


Eperance ilianza kwa kuchapwa mabao 3-1 katika mchezo wa fainali ya kwanza uliochezwa Misri, kabla ya kushinda mabao 3-0 katika fainali ya pili na kutwaa taji hilo kwa ushindi wa jumla wa mabao 4-3.


Timu hiyo ilianzia moja kwa moja kwenye hatua ya makundi ya michuano hii ambapo walipangwa kundi B na timu za Horoya ya Guinea, Orlando Pirates ya Afrika Kusini na FC Platinum ya Zimbabwe.


Wababe hao wa Tunisia walizindua kampenizi zao kwa kutoka sare ya bao 1-1 na Horoya ugenini, ikaichapa FC Platinum mabao 2-0 nyumbani, ikilazimisha suluhu na Orlando Pirates ugenini.


Katika mkondo wa pili, timu hiyo ilianza kwa kuichapa mabao 2-0 Orlando katika mchezo wa marudiano nyumbani, ikiitandika mabao 2-0 Horoya nyumbani kabla ya kumaliza kwa kuilaza FC Platinum mabao 2-1 ugenini.
Licha ya kumaliza kama timu iliyokusanya pointi nyingi katika hatua ya makundi, lakini timu hiyo imeshinda michezo mitatu ya nyumbani, mmoja ugenini na kutoka sare miwili, ikifunga mabao tisa na kuruhusu mabao mawili tu.


TP MAZEMBE
Wababe hao wa zamani wa michuano hiyo, walianzia raundi ya kwanza kwa kucheza na Zesco United ya Zambia, ambapo mchezo wa kwanza ilishinda bao 1-0 nyumbani, kabla ya kulazimisha sare ya bao 1-1 ugenini na kutinga hatua ya makundi kwa ushindi wa jumla ya mabao 2-1.
Timu hiyo ilipangwa katika kundi C na timu za Costantine ya Algeria, Club African ya Tunisa na Ismailia ya Misri.


Mazembe ilizindua kampeni zake kwa kuichapa Ismaily mabao 2-0 nyumbani, ikichapwa mabao 3-0 ugenini na Constatine, ikahitimisha michezo ya mkondo wa kwanza kwa kuifumua Club African mabao 8-0.


Ilianza mkondo wa pili kwa kurudiana na Club African na kulazimisha suluhu, ikitoka sare ya bao 1-1 na Ismailia ugenini, kabla ya kumaliza kwa kuilaza Constantine mabao 2-0 nyumbani.


Katika michezo hiyo minane, Mazembe imeshinda mechi nne nyumbani na moja ugenini, huku pia ikipoteza mchezo mmoja ugenini na kutoka sare miwili.

Hizo ni timu ambazo moja wapo itakutana na Simba SC baada ya kuchezeshwa droo leo huko Cairo nchini Misri.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
591,000SubscribersSubscribe

Latest Articles