Bethsheba Wambura, Dar es Salaam
Serikali imesema inatarajia kupokea ndege nyingine aina ya Boeing Dreamliner yenye uwezo wa kubeba abiria 262 iliyotengenezwa nchini Marekani.
Dreamliner hiyo ambayo itakuwa ni ya pili baada ya ile ya kwanza ya Boeing 787-8 Dreamliner iliyotua hapa nchini Julai 8, mwaka jana amabyo hadi sasa inafanya safari zake Entebbe nchini Uganda, Bujumbura nchini Burundi na Visiwa vya Comoro.
Akizungumza katika mapokezi ya ndege mpya aina ya Airbus 220-300 Waziri wa Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano, Isack Kamwelwe amesema Serikali ilipanga kulifufua Shirika la Ndege nchini (ATCL) kwa kununua ndege mpya Saba.
“Rais Magufuli alipoingia madarakani aliahidi kuifufua ATCL kwa kununua ndege saba lakini juzi kanipigia simu kuniagiza tununue nyingine ziwe nane kabisa, ”amesema Waziri Kamwelwe.
Naye Rais Magufuli amesema pamoja na kuwa aliahidi kununia ndege saba na nyingine zimeshawasili lakini huo si mwisho kwani ana mpango wa kuagiza ndege nyingi zaidi.
“Nataka mjue kuwa ndege hii tunayopokea leo sio ya mwisho nataka kununua ndege nyingine zaidi ambazo zitakuwa zinapishana katika masafa ndani na nje ya Afrika,” amesema Rais Magufuli.
Hadi sasa ndege sita zilizonunuliwa na Serikali zimeshawasili hapa nchini ukiachana na hizo za Airbus 220-300 na Dreamliner nyingine ni Bombadier Dash 8 Q400 tatu zenye uwezo wa kubeba airia 76 kila moja.