27.1 C
Dar es Salaam
Thursday, January 2, 2025

Contact us: info@mtanzania.co.tz

Dogo Janja endelea kuwaonyesha njia mastaa wenzako

NA CHRISTOPHER MSEKENA

WATU wengi mashuhuri katika sekta ya sanaa wanalazimika kuigiza maisha ya hadhi ya juu ili kulinda nafasi zao kama wasanii mbele ya jamii na wawekezaji.

Ndiyo maana utaona mastaa wengi hapa Tanzania wanaishi maisha mazuri katika majumba ya kifahari huku wakitembelea magari ya bei ghali, lakini ukifuatilia utabaini ukweli kuwa nyumba hizo ni za wahisani na hizo gari ni za kuazima.

Tumeona uongo wa wasanii wengi pale ambapo wanafariki dunia na kwenda kuzikwa nyumbani kwao walikozaliwa, utaona wazazi wao wanaishi maisha ya dhiki tofauti na ukubwa wa majina ya watoto wao huku mjini.

Kwa mastaa werevu lazima waweke mazingira mazuri nyumbani kwao ili hata likitokea jambo lolote la dharura wawe vizuri. Binafsi nimevutiwa na alichokifanya rapa, Abdul Chande ‘Dogo Janja’, nyumbani kwao Sombetini, Arusha.

Dogo Janja amefanikiwa kumjengea mama yake nyumba nzuri ya awali jambo ambao limepongezwa na wengi nikiwamo mimi huku wengine wachache wakimponda.

Ni kawaida kupokea mitazamo tofauti kwani inakupa changamoto ya kufanya kitu kizuri zaidi ya mwanzo lakini kwa hili Janjaro anastahili pongezi, amempa utulivu mama yake mzazi ambaye aliteswa na kero katika nyumba za kupanga.

Dogo Janja nampongeza kwa sababu bila shaka amewatoa gizani mastaa wengi wala bata hapa mjini na sasa wataanza kukumbuka makwao kwa kuwafanyia mambo mazuri wazazi wao.

Rapa huyo si kama ana fedha nyingi kwa sababu kama fedha ameanza kuzipata miaka miwili nyuma alipotoa wimbo wake My Life, ndiyo maana amepata pongezi nyingi kwa kitu ambacho amekifanya kwani tunaona mastaa wa muda mrefu hapa mjini hawajaweza kufanya hivyo.

Pia mbali na kumpa furaha mama yake, Janjaro amerudisha fadhila kwenye jamii katika shule ya msingi aliyosoma, Unga Limited huku akiahidi kuwawezesha wanafunzi watakaofanya vizuri katika masomo yao.

Hilo pia si jambo dogo, ni kitu kinachopaswa kuwafungua macho mastaa wetu kushiriki katika masuala ya kijamii kwa kutoa kidogo walichonacho. Janjaro anastahili pongezi nyingi kuliko kubezwa wakati tunaona wasanii wengi hawana kawaida ya kufanya hivyo.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
593,000SubscribersSubscribe

Latest Articles