NA KOKU DAVID, DAR ES SALAAM
MKOA wa Dodoma umetajwa kuwa na viashiria vya juu katika maambukizi ya Ukimwi ikilinganishwa na mikoa mingine.
Hali hiyo imetokana na kuwepo kwa vitu kadhaa vinavyowakutanisha vijana vikiwamo vyuo na sehemu za starehe.
Akizungumza na MTANZANIA jana jijini Dar es Salaam, Mratibu wa Programu za Kanda za Afrika, Renatus Kihongo alisema utafiti uliofanywa mwaka 2012 unaonesha vijana wengi katika Manispaa ya Dodoma wanatumia muda mwingi kwenye starehe, jambo ambalo ni linatishia uwepo wa maambukizi ya ugonjwa huo.
Utafiti huo uliofanywa na Tume ya Kudhibiti Ukimwi Tanzania (TACAIDS) viashiria vya maambukizi ya ukimwi vipo juu kwa vijana kati ya miaka 15 hadi 24 ambapo wanafunzi wa vyuo vikuu ndio wanaoonekana kuwepo katika viashiria hivyo.
Kihongo alisema Mkoa wa Dodoma kitaifa upo katika nafasi ya 22 kwa kuwa na maambukizi ya Ukimwi.
“Mara nyingi sehemu yoyote yenye maendeleo inakwenda sambamba na viashiria vya maambukizi ya Ukimwi kutokana na kuwepo na muingiliano mkubwa wa watu ambao baadaye hujenga uhusiano.
“Dodoma ni makao makuu ya nchi, hivyo kuna maendeleo na ni lazina viashiria vya maambukizi ya Ukimwi vitaongezeka lakini TACAIDS imeamua kuelekeza nguvu katika mkoa huo ili kuhakikisha inadhibiti ili visije vikamaliza nguvu kazi ya taifa,”alisema Kihongo.
“TACAIDS kwa kushirikiana na Mgodi wa Dhahabu wa Geita (GGM) huwa tunafanya harambee kupitia upandaji wa Mlima Kilimanjaro ambapo mwaka huu tumepanga fedha zilizopatikana zitumike kwa kuanzisha program maalumu ambayo itasaidia kufanya kampeni kwa njia ya vyombo vya habari kuhu Ukimwi katika Mkoa wa Dodoma,” alisema.