Na Ramadhan Hassan,Dodoma
KLABU ya Soka ya Dodoma Jiji inayoshiriki Ligi Kuu Tanzania Bara (TPL) imeingia makubaliano ya udhamini wa miaka mitatu na kampuni michezo ya kubashiri Barani Afrika ya 10BET.
Hafla ya makubaliano hayo, uliokwenda sambamba na utambulisho wa jezi za msimu wa 2021/2022 za timu hiyo, umehudhuriwa na madiwani wa Jiji la Dodoma,wakiongozwa na Naibu Meya Emmanuel Chibago,Mkuu wa Wilaya ya Dodoma Mjini,Jabir Shekimweri.
Pia alikuwepo Mbunge wa Jimbo la Dodoma Mjini,Anthony Mavunde pamoja na mashabiki wa timu hiyo.
Akizungumza wakati wa utambulishaji wa kampuni hiyo leo Septemba 27,2021 Jijini Dodoma,Katibu Mkuu wa timu ya Dodoma Jiji, Fortunatus John amesema kupitia makubaliano hayo kampuni hiyo kwa msimu wa kwanza ndio itakayogharamia vifaa mbalimbali vya michezo vitakavyotumika katika mazoezi na mechi.
“Uongozi wa 10BET unaamini klabu yetu itakuwa ni mshirika mzuri kwao na mkataba huu utasaidia kuwafikia mamilioni ya wateja kirahisi,”amesema.
Kwa upande wake,Mkuu wa Wilaya ya Dodoma Mjini,Shekimweri amelitaka benchi la ufundi kuendana na uwekezaji ambao uongozi wa timu hiyo umekuwa ikiufanya kwa kuhakikisha timu inapata matokeo katika michezo yake.
“Huu ni uwekezaji mkubwa malengo yetu sisi sasa ni kuwa katika ‘Top 2’ hapa hakuna Usimba wala Uyanga,Dodoma Jiji Fc kwanza, hivyo benchi la ufundi ni lazima liufanyie kazi uwekezaji huu katika matokeo kwa timu kufanya vizuri,”amesema.
Mbunge wa Jimbo la Dodoma Mjini, Mavunde amesema Dodoma Jiji kwa sasa wamejipanga na hakuna timu ambayo itatoka katika Uwanja wa Jamhuri ambapo ametoa rai kwa mashabiki kujitokeza kwa wingi viwanjani kuishangilia timu hiyo.