Na Esther Mnyika, Mtanzania Digital
Chuo cha Bahari Dar es Salaam (DMI) kwa kushirikiana na Reginal Maritane University cha nchini Ghana wameandaa kongamano la tatu la mwaka la Kimataifa litakalozungumzia dhana nzima ya uchumi wa buluu.
Akizungumza leo Machi 15,2024 jijini Dar es Salaam na waandishi wa habari Mkuu wa Chuo cha DMI, Dk. Tumaini Gulumo amesema kongamano hilo,linatarajiwa kufanyika nchini kuanzia Julai 4 – 5, 2024 jijini kwenye Ukumbi wa Mikutano wa Kimataifa wa Mwalimu Nyerere (JNICC) huku nchi mbalimbali duniani zikitarajiwa kushiriki.
“Chuo Chetu kikishirikiana na kile cha Reginal Maritane University cha nchini Ghana kimeandaa mkutano huo wenye lengo la kutafsiri dhana nzima ya uchumi wa buluu ambapo Tanzania imepewa heshima kubwa ya kuandaa kongamano hili tunajivunia,” amesema Dk.Gulumo.
Amesema mbali na mambo mengine yatakayo jadiliwa kwenye kongamano hilo ni pamoja na usalama wa bahari ikiwemo uharamia, matumizi mabaya ya baharini ikiwemo uharibifu wa mazingira.
Aidha Dk. Gulumo ametoa ufafanuzi juu ya dhana nzima ya uchumi wa buluu ikiwemo shughuli nyingi zinazofanyika baharini kama sekta ya uchukuzi,uchimbaji wa mafuta na gesi, uvuvi, utalii na kilimo cha mwani na nyinginezo.
Amesema hiyo ni mara yao ya tatu kuandaa kongamano kama hilo, wakianzia mwaka 2022 na kusisitiza kuwa kwa sasa wanahitaji utashi wa kisiasa kwani serikali zote mbili zimekuwa zikisisitiza ukuaji wa uchumi wa buluu ili kutekeleza dhana nzima ya uchumi huo.
Ametaja madhumuni makubwa ya kongamano hilo mwaka huu ni kutoa fursa kwa wadau wa uchumi wa buluu kukutana,kujadiliana, na kubadilishana uzoefu ili kukuza uchumui wa buluu.
Ameongeza kuwa DMI ndio chuo pekee hapa nchini kilichopewa mamlaka kumsimamia mambo yote yanayohusu uchumi wa buluu bila kuangalia vyanzo vingine vya maji vilivyopo nchini.
Pia Gulumo amezitaka sekta mbalimbali kushiriki kongamano hilo, zikiwemo wizara ambazo zinahusika moja kwa moja kwenye sekta ya uchumi wa buluu.
Ametaja nchi ambazo hadi sasa zimethibitisha kushiriki kongamano hilo kuwa ni pamoja na Ghana Kenya,Uganda Korea ambazo zitashiriki mkutano huo.