28.3 C
Dar es Salaam
Wednesday, February 21, 2024

Contact us: [email protected]

DK. TIZEBA: UVUVI HARAMU NI UHUJUMU UCHUMI

uvuvi-haramu

Na Mwandishi Wetu,

SERIKALI imechoshwa na mwenendo wa mapambano na wale wanaofanya uvuvi haramu na hivyo  kutaka kubadilisha sheria ya uvuvi ili ziwe na meno kwa kutoa adhabu kubwa kwa  wakosaji.

Sekta ya uvuvi nchini inatawaliwa na sheria kuu mbili za Sheria ya Uvuvi ya mwaka 2003 na Sheria ya Mamlaka ya Kusimamia Uvuvi wa Bahari Kuu ya mwaka 2009.

Sheria hizo zimepitwa na wakati kwani zinatoa adhabu ndogo  na matendo ya wavuvi haramu yamepita ya uvuvi na kuwa ya uhujumu uchumi kwa kuua mazalio ya samaki na kuharibu miundombinu ya uchumi endelevu na hivyo kuhitaji mtazamo mpya na mkakati wa ushindi mahakamani si  ngonjera isiyo ya tija.

Mikakati hiyo ya Serikali imekuja baada ya sheria na kanuni zilizopo kushindwa kupambana kikamilifu na vitendo vya uvuvi haramu vinavyotishia ukuwaji wa sekta ya uvuvi nchini.

Serikali itafanya mabadiliko ya sheria zinazosimamia uvuvi kwa kuyaainisha baadhi ya makosa ya uvuvi haramu kuwa ni ya uhujumu uchumi, ili kuongeza adhabu iwe kali kwa watu wanaotiwa hatiani kwa makosa hayo.

Waziri wa Kilimo, Mifugo na Uvuvi, Dk. Charles Tizeba, amesema wataalamu wa wizara hiyo wamebainisha upungufu uliopo kwenye sheria zilizopo na kilichobaki ni kuwasilisha mabadiliko hayo mbele ya Bunge ambalo litaamua kwa kiasi gani wataweza kuwabana  wavuvi walio waharibifu na wavunjaji sheria.

Akifafanua kuhusu hali halisi  alisema amesikitishwa kuona kuwa vitendo vya uvuvi haramu havikomi licha ya Serikali kupambana navyo kwa kuwa adhabu zinazotolewa na sheria zilizopo haziwaogopeshi wavuvi haramu ambao shughuli zao huwaingizia mamilioni ya fedha pale wanapoamua kufanya uhalifu tena kwa muda mfupi  tu na kwa gharama  ndogo sana ya baruti.

Dk. Tizeba alisema hayo wakati wa ziara ya kushtukiza kwenye Soko la Samaki la Feri ambapo alishuhudia mzigo wa tani moja na nusu za samaki walizozikamata sokoni hapo Dar es Salaam zenye thamani ya mamilioni zikiwa zimevuliwa kwa mabomu na wavuvi hao kuacha mzigo walipoona wako hatarini kukamatwa na mamlaka za Serikali na hivyo kutoroka kuwa ni dalili tosha za kutoogopa mkono mrefu wa sheria.

Dk. Tizeba alitanabaisha kuwa  baadhi ya samaki hao walivuliwa katika kina kirefu wakionesha wavuvi hao wana uwezo mkubwa wa kifedha  na hivyo kutambua kuwa wakipelekwa mahakamani kwa sheria zilizopo adhabu yao ni kifungo miezi sita au faini yao ni Sh 200,000.

“Kiwango hiki ni kama unawaambia waende walipe ushuru wa Serikali kupitia Mahakama kwa sababu mzigo wanaovua ni mkubwa unaozidi hata thamani ya shilingi milioni 18,” alisema.

Akionesha  kukerwa na hali hiyo, Dk. Tizeba alisema hakuna namna nyingine ya kukabiliana na vitendo hivyo haramu zaidi ya kuweka adhabu kali kwa wanaotiwa hatiani kwa kuyaainisha baadhi ya makosa ya uvuvi haramu kuwa ni uhujumu uchumi au ugaidi wa silaha (terrorism) kwa vile wanatumia milipuko  au mabomu na kumaliza mazalio ya samaki  na kutishia wafanyakazi wa Serikali wanaofuatilia masuala hayo.

Kwa masikitiko, Dk. Tizeba  alisema:  “Ninapenda kusema kuwa Serikali imeshindwa sehemu kubwa ya kesi zilizohusisha matumizi ya mabomu katika uvuvi kutokana na  kutokuwepo maana nzuri ya vilipuzi na vinavyolipuliwa na namna ya kuwasilisha ushahidi wake kikamilifu, jambo linalopunguza kasi ya kutokomeza vitendo hivyo dhalimu kwa rasilimali na mazingira.”

Anasema adhabu za sasa hazimfanyi mtu aogope na kuacha uvuvi haramu lakini kama adhabu itaongezwa na kuwekwa kifungo cha miaka 15 kwa atakayetiwa hatiani, wengi wataogopa.

Waziri Tizeba anaamini kuwa hayo yakifanywa sanjari na uelimishaji umma juu ya madhara ya uvuvi haramu Wizara itafanikiwa kutokomeza kabisa vitendo hivyo vya uvuvi haramu.

Kuthibitisha  msimamo mkali wa Serikali kuhusu makosa hayo, Waziri alisema Serikali inaendelea na operesheni zake za  kudhibiti uvuvi haramu katika mnyororo wote wa thamani  kwa maana kutoka kwa watengenezaji nyavu haramu, wanaoziingiza nchini, wasafirishaji, wavuvi hadi kwa wachuuzi wa samaki waliovuliwa kiharamu na wanunuzi wao.

Hivi basi serikali imelenga vita hiyo kwa wahusika wote na popote walipo  ili kuifanya iwe juhudi ya pamoja na kuainisha kero zake.

Dk. Mathias Igulu, ni mtaalamu wa masuala ya bahari kutoka shirika la kimataifa la WWF, ambaye ni mratibu wa masuala ya bahari wa shirika hilo alisema uvuvi haramu unaweza kukomeshwa iwapo kila mmoja atawajibika wakiwamo wamiliki wa hoteli, viwanda na wananchi kukataa kununua samaki wadogo au wakubwa waliovuliwa kwa njia haramu. Mgomo wa walaji ni muhimu kwa shughuli yoyote ya kiuchumi kwani bila wao hakuna biashara.

Dk. Igulu amesema uvuvi haramu unatishia mustakabali wa vizazi vijavyo kwa kuwa matumizi ya mabomu na sumu huharibu mazalia na makazi ya samaki kwa muda mrefu na hivyo si rahisi kurudia hali ya asilia.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
583,000SubscribersSubscribe

Latest Articles