Zaituni Kibwana, Dar es Salaam
KUELEKEA uchaguzi wa Yanga SC, majina matano ya watu maarufu kwenye mchezo wa soka nchini, Dk Jonas Tiboroha, Imani Madega, Yono Kevela, Titus Osoro na Mbaraka Igangula wamejitokea kuchukua fomu kugombea nafasi ya unyekiti wa klabu hiyo iliyokuwa inashikiliwa na mfanyabiashara Yusuph Manji.
Uchaguzi huo ambao umepangwa kufanyika Januari 13 mwakani, awali ulipangwa Novemba 14 kuwa mwisho wa uchukuaji wa fomu za kugombea nafasi mbalimbali za uongozi katika klabu hiyo lakini kwa sasa tarehe hiyo imesogezwa mbele hadi November 19 mwaka huu.
Akizungumza na MtanzaniaDigital, wakili Ally Mchungahela amesema idadi ya waliojitokeza kuchukua fomu ya kugombea nafasi mbalimbali wanafika 21.
Wakili huyo amesema waliojitokeza kuwania nafasi za ujumbe wapo 16 ambao ni Dominic Francis, Pindu Luloyo, Said Baraka na Shafii Amri.
Wengine ni mjumbe wa zamani Musa Katabalo, Salim Seif, Silvester Haule, Benjamin Jackson na Hamad Islam.
Wajumbe wengine ni Ally Msigwa, Arafat Haji, Geoffrey Mwita, Frank Kalo kola, Ramadhani Said, Leonard Marongo na Salum Chota.
Uchaguzi huo umepangwa kufanyika January 13, 2019 baada ya Baraza la Michezo Tanzania (BMT) na Shirikisho la Soka Tanzania (TFF) kuitaka Yanga kuitisha uchaguzi wake kwa ajili ya kujaza nafasi zilizo wazi ikiwemo ya aliyekuwa mwenyekiti wao Yusuph Manji aliyeandika barua ya kujiuzulu Mei 2017.