27.1 C
Dar es Salaam
Thursday, January 2, 2025

Contact us: info@mtanzania.co.tz

Dk. Slaa: Tumejiandaa urais 2015

Dk. Wilbrod Slaa
Katibu Mkuu wa Chadema, Dk. Wilbrod Slaa

Na Esther Mbussi, Dar es Salaam

KATIBU Mkuu wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema), Dk. Willibrod Slaa, amesema chama chake kimejipanga vizuri kukabiliana na mgombea yeyote wa urais atakayeteuliwa na Chama Cha Mapinduzi (CCM), katika uchaguzi mkuu ujao.

Amesema kwamba, pamoja na CCM kubuni mbinu ya kupandikiza baadhi ya watu wanaoeleza jinsi wanavyotaka kuwania urais, Chadema hawatakurupuka kutangaza mgombea wao kwa sababu wanajua madhara ya kufanya hivyo mapema.

Dk. Slaa alitoa kauli hiyo mwishoni mwa wiki alipokuwa akizungumza na MTANZANIA Jumatatu juu ya masuala mbalimbali ya kitaifa, hali ya kisiasa nchini na uchaguzi mkuu ujao.

“Kwetu sisi suala la urais si kipaumbele ingawa tunawasikia wenzetu wameanza kugombana kuhusu urais na umri wa kugombea. Sisi tunasema hatutishiki na yeyote watakayemteua, tunaamini hakuna mgombea tishio katika CCM, yaani hata wamsimamishe Malaika tutakabiliana naye, jambo la msingi hapa ni kuweka misingi ya chama.

“Kabla ya uchaguzi mkuu wa mwaka 2010, nilikuwa sielewi maneno ya Baba wa Taifa, Mwalimu Julius Nyerere alipokuwa akihoji ni kwanini watu wanagombea kwenda Ikulu.

“Nimezunguka nchi nzima kwa magari, daladala na ndege si kwa bahati mbaya bali ni kwa makusudi ili kujua mambo yakoje huko vijijini na nikatambua hatuna barabara wala trekta la kukuvuta ukikwama barabarani.

“Leo unaniuliza Dk. utagombea urais, kwa raha gani iliyoko Ikulu, kuna nini huko, wanaokimbilia Ikulu aidha wanaficha ufisadi wao au wanakwenda kuimarisha biashara zao.

“Pia ni kwamba, Chadema hatuandai urais kwenye magazeti, sisi hatuna fedha, hatuna nyenzo ila tuna moyo mpana wa kutusaidia kumkomboa Mtanzania maskini kwa sababu hatuogopi risasi wala sumu.

“Kwa maana hiyo, wakati ukifika mgombea wetu wa urais atatangazwa na tutamteua mtu makini mwenye upendo, muadilifu na mwenye utashi wa kuwatumikia Watanzania kwa moyo,” alisema Dk. Slaa.

Ili kuhakikisha Chadema kinashika dola, alisema kwa sasa chama kina mikakati ya kujiimarisha kwa kuwa na matawi yenye mabalozi kama ilivyo kwa CCM.

Hadi sasa alisema chama chao kina misingi 250 inayotakiwa kukamilika kabla ya uchaguzi mkuu ingawa hadi sasa wamekamilisha misingi 196.

“Tulifuta uchaguzi mara tatu, mara mbili mwaka 2012 na mara moja mwaka jana, hiyo ni kwa sababu huko chini hatukuwa na misingi na hii ilikuwa ni sehemu ya maandalizi ya kuelekea katika uchaguzi mkuu mwakani baada ya kukamilisha uchaguzi wa ndani wa chama chetu.

Kuhusu Katiba Mpya

Akizungumzia kuhusu Katiba Mpya, Dk. Slaa alisema haiwezi kupatikana kwa wakati uliokusudiwa kwa sababu CCM haikuwa na dhamira ya dhati na Katiba hiyo kwa kuwa kuna viashiria vya rushwa na upotoshaji katika mchakato huo.

“Majuzi niliwasikia kinamama wasomi wakisema wanataka usawa katika Katiba Mpya na kwamba si lazima kuwepo na idadi ya Serikali.

“Hawa ni wasomi wasioelewa vema msingi wa Serikali, huwezi kuzungumza chochote bila kuanza na muundo wa Serikali, huu ndiyo msingi, hata Sitta (Samuel Sitta, Mwenyekiti wa Bunge Maalumu la Katiba) mwenyewe alisema huo ndiyo msingi.

“Hivi kweli wasomi wetu wanashindwa kutambua mambo, haya ni matokeo ya mambo yaliyokwisha tangazwa awali,” alisema.

- Advertisement -

Related Articles

2 COMMENTS

  1. Dr. Slaa amesema kuwa katiba haiwezi kupatikana kwa wakati uliotarajiwa. Hilo ni kweli na linasikitisha sana. Haya yote yanatokana na kuwa na malengo binafsi(Personal Gain)Wananchi walikuwa wanasubiri kwa hamu kubwa kupata katiba mpya lakini wameangushwa na misimamo ambayo haina tija kwa taifa hili.

  2. Hapa Slaa amezungumzia kitu muhimu sana – kutengeneza jumbe kama zile za CCM. Ni dhahiri sasa CHADEMA wameanza kuelewa kuwa “grassroot administration and managemen” ni kitu muhimu sana katika kufanikisha shughuli zote zikiwemo za uchaguzi. Menejimenti hiyo hiyo ndiyo ilikuwa ikitumiwa na TANU na baadae CCM kuleta maendeleo kwa wananchi. Wapinzani akiwemo Augustine Mrema walipinga sana balozi hizi kwenye miaka ya 90 kwa kuwa ni mfumo wa uongozi wa CCM. Nchi kadhaa zimeiga mfumo huu baada ya kuona faida zake. Ifike wakati serikali ibuni mfumo mpya wa utawala katika ngazi hii utakaohusisha watu wote bila kujali vyama. CCM bado ina nguvu kubwa sana kupitia mfumo huu na si ajabu kama itashinda kwa vishindo.

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
593,000SubscribersSubscribe

Latest Articles