24.9 C
Dar es Salaam
Monday, November 18, 2024

Contact us: [email protected]

Dk. Shein apigia chapuo teknolojia ya habari

MWANDISHI WETU – ZANZIBAR

RAIS wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, Dk. Ali Mohamed Shein, amesema teknolojia ya habari na mawasiliano ina nafasi kubwa ya kuleta mabadiliko ya maendeleo katika mabunge ya nchi za Jumuiya ya Madola.

Aliyasema hayo jana katika ufunguzi wa mkutano wa 50 wa Chama cha Mabunge cha Jumuiya ya Madola (CPA) Kanda ya Afrika, unaofanyika Mbweni, nje kidogo ya mji wa Unguja.

Dk. Shein alisema iwapo teknolojia ya habari na mawasiliano itatumika ipasavyo, hasa katika kuimarisha kanzi data mbalimbali, hatua hiyo itarahisisha suala zima la kufanya maamuzi kwa wakati na kuweza kufikia malengo yaliyokusudiwa.

Alisema kuwa uendeshaji wa Bunge kwa kutumia njia za kisasa kunawaweka karibu zaidi wabunge na wananchi.

“Jambo hilo linatoa fursa pana zaidi kwa wananchi ya kutoa maoni yao na hoja mbalimbali za maendeleo zinazogusa maisha yao ya kila siku,” alisema Dk. Shein.

Alieleza kuwa Bunge Mtandao ni nyenzo nzima ya kupunguza gharama za mambo mbalimbali kama vile usafiri sambamba na kuokoa muda.

“Juhudi zinazochukuliwa na nchi wananchama wa jumuiya hiyo za kuimarisha Bunge Mtandao, lazima ziende sambamba na juhudi za uhamasishaji wa teknolojia ya habari katika skuli zilizo katika majimbo yao na nchi nzima kwa jumla.

“Nafahamu kwamba matumizi ya teknolojia ya mawasiliano ikiwemo mitandano ni muhimu sana katika utekelezaji wa majumuku ya wabunge duniani, likiwemo suala la utungaji wa sheria, kuwasilisha hoja za wananchi pamoja na kusimamia utekelezaji wa shughuli za Serikali,” alisema.

 Dk. Shein alitumia fursa hiyo kupongeza juhudi zinazochukuliwa na wabunge pamoja na wajumbe wa Baraza la Wawakilishi za kushirikiana na uongozi wa skuli mbalimbali zilizomo katika majimbo yao kuhamasisha utoaji wa elimu ya habari na mawasiliano.

Alisema kuwa Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar imetekeleza mradi mkubwa wa Serikali Mtandao ambao aliuzindua rasmi Januari 2013.

Aliwashukuru wajumbe wa mkutano huo kwa uamuzi wao kufanya mkutano huo mkuu wa 50 Zanzibar na kuwapongeza Spika wa Bunge, Job Ndugai na Spika wa Baraza la Wawakilishi, Zubeir Ali Maulid kwa matayarisho mazuri na kuufanikisha.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
591,000SubscribersSubscribe

Latest Articles