Na Benny Mwaipaja, Dar es Salaam
Waziri wa Fedha na Mipango, Dk. Mwigulu Nchemba, amewahakikishia wafanyabiashara hapa nchini kuwa Wizara yake itahakikisha inarejesha taswira na mahusiano mazuri nao katika masuala yakodi ili kuboresha mazingira ya ufanyaji biashara na kusisimua uchumi wa nchi.
Dk. Nchemba ametoa ahadi hiyo Ikulu jijini Dar es Salaam leo Aprili 6, 2021 alipozungumza na vyombo vya habari baada ya tukio la kuapishwa kwa Makatibu Wakuu na Naibu Makatibu Wakuu pamoja na viongozi wa Taasisi, tukio lililofanywa na Rais wa Tanzania, Samia Suluhu Hassan.
“Tutatengeneza vyanzo vipya vya makusanyo ili mzigo wa kodi usibebwe na wachache kwa sababu kadri mzigo unavyobebwa na wengi ndivyo nafuu inavyopatikana, hatua itakayowafanya wafanyabiashara wengi kulipa kodi kwa hiari,” alieleza Dk. Nchemba.
Aidha, Dk. Nchemba aliyeanza kazi hivi karibuni kama Waziri wa Fedha na Mipango, amesema kuwa amekutana na wataalam wa Wizara yake na kuwaagiza wakutane na wenzao wa Serikali ya Mapinduzi Zanzibar ili kujadili namna ya kutatua changamoto za Muungano na kwamba anaamini zitapatiwa ufumbuzi.
“Shida ya watu wetu wengi wanapojadili masuala haya hawatuambii walipokwama, kwahiyo niliwaambia watubainishie wanapokwama ili tupate ufumbuzi wa jambo hilo baada ya hapo tutakaa Wizara tatu, Wizara ya Fedha na Mipango, Wizara ya Fedha na Mipango Zanzibar na Ofisi ya Makamu wa Rais na kufanya uchambuzi wa kina,” alifafanua Dk. Nchemba.
Kuhusu udhibiti wa matumizi wa Fedha za Umma, Dk. Nchemba amesema kuwa Wizara yake itatumia mifumo ya fedha iliyobuniwa kudhibiti matumizi ya Serikali na kuboresha mifumo ya ukusanyaji wa mapato ili iwe michache lakini yenye ufanisi pamoja na kuimarisha masuala ya utawala katika kukusanya mapato na matumizi yake ili fedha hizo zilete matokeo yaliyokusudiwa.
Waziri wa Fedha na Mipango alishuhudia kuapishwa kwa watendaji wake wapya, akiwemo Katibu Mkuu na Mlipaji Mkuu wa Serikali, Emmanuel Tutuba na Naibu Katibu Mkuu wa Wizara hiyo, Dk. Khatibu Kazungu ambao wameapishwa na Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mher. Samia Suluhu Hassan, Ikulu, jijini Dar es Salaam.