25.8 C
Dar es Salaam
Tuesday, November 26, 2024

Contact us: [email protected]

DK. MWAKYEMBE: MWISHO WA MABONDIA KUDHULUMIWA UMEFIKA

Na ADAM MKWEPU-DAR ES SALAAM        |     


KUKOSEKANA chombo makini cha kusimamia mchezo wa masumbwi nchini kumesababisha ushindwe kupiga hatua, badala yake umezidi kurudi nyuma na kupoteza mwelekeo.

Ukosefu wa chombo makini umesababisha kuwapo kwa migogoro ya mara kwa mara ambayo imeathiri ukuaji wa mchezo huu, ambao huko nyuma ulikuwa ukipendwa na Watanzania wengi, lakini kubwa ulililetea sifa Taifa letu la Tanzania.

Kupitia mchezo huu, Tanzania iliweza kujitangaza vema nje ya mipaka yake kutokana na wabondia wake kutamba katika mapigano ya kimataifa.

Mabondia walikuwa wakijitoa kwaajili ya taifa lao na taasisi mbalimbali, hasa majeshi zilikuwa mstari wa mbele kuwaunga mkono.

Majina kama Rashid Matumla, marehemu, Stanley Mabesi ‘Ninja’ na Michael Yombayomba, ni baadhi ya mabondia walioipeperusha vema Bendera ya Tanzania katika medani ya kimataifa, kutokana na kushinda mataji kadhaa.

Walichokifanya mabondia hao kinaendelea kuenziwa na kukumbukwa na wadau wa soka hapa nchini.

Kizazi cha sasa cha akina Francis Cheka kimejitahidi kupambana, lakini kimeshindwa kufanya yale yaliyofanywa na Matumla na wenzake nje ya mipaka ya Tanzania.

Hata hivyo, baada ya taasisi, hasa za kiserikali kuacha kusapoti mchezo huu, umeathirika kwa kiasi kikubwa.

Hakuna tena vipaji vipya vya maana ambavyo vimekuwa vikizalishwa, kwakuwa mabondia chipukizi wamekuwa hawapati mahitaji ya msingi yanayoweza kuwafanya wawe bora zaidi.

Ukata ni tatizo sugu kwa sasa katika mchezo wa masumbwi na kuhatarisha maendeleo yake.

Ukweli ni kwamba, mchezo wa ngumi umeshuka thamani machoni mwa Watanzania na wadau wa mchezo huo na kuondoa heshima yake kwa waliokuwa wakiupenda.

Mapromota hawapendani, mabondia wanafanyiana figisu, viongozi wa mashirikisho ndiyo usiseme, kila mmoja ana kundi au upande wake, bila kujali kama unafanya vizuri au vibaya.

Waziri wa Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo, Dk. Harrison Mwakyembe, ameonyesha nia ya dhati katika kurejesha heshima ya mchezo huu pamoja na kutatua migogoro iliyodumu kwa kipindi kirefu.

Tangu mwishoni mwa mwaka 2017, Waziri Mwakyembe amekuwa na vikao mfululizo na wadau wa mchezo huu, akilenga kutafuta mwarobaini wa matatizo yanayoufanya usipige hatua.

Tayari Dk. Mwakyembe ameunda mfumo mpya wenye lengo la kulinda maslahi ya mabondia na wadau wengine wa mchezo huu.

Mwakyembe ameunda Kamati ya Mpito ambayo itashirikiana na Baraza la Michezo la Taifa (BMT), kuhakikisha kila kitu kinakwenda vizuri katika mchezo huu.

BMT itahakikisha hakuna bondia anayesafiri nje ya Tanzania kupigana bila kupata kibali maalumu kutoka kwake.

Waziri Mwakyembe pia yupo katika hatua ya mwisho ya kukabidhi katiba, ambayo itakuwa msingi utakaosimamia mchezo wa ngumi za kulipwa hapa nchini.

Akizungumza hivi karibuni wakati akipokea mrejesho uundwaji wa katiba mpya itakayosimamia mchezo wa masumbwi, Mwakyembe anasema:

“Naapa kwa Mungu nitausafisha mchezo wa ngumi na hakuna atakayeweza kupambana na Serikali.

“Ukiwa na chombo mahususi cha kusimamia mchezo huu, hakuna migogoro itakayojitokeza, haya yote yanayotokea yanatokana na kila chama cha ngumi kuwa na uhuru wa kufanya wanavyojisikia”.

Mwakyembe anasema kamati ya mpito aliyoiunda inalengo la kusaidia kupata katiba mpya ya mchezo wa ngumi za kulipwa nchini.

Anasema kilichobaki kwa sasa ni kuitisha mkutano wa wadau wa masumbwi ambao unatarajiwa kufanyika Juni, mwaka huu, ili kuikabidhi katiba hiyo.

“Haya yote yanafanyika kwa kuwa mchezo wa ngumi umegubikwa na vitendo vya jinai na vurugu.

“Katika vitendo, hivyo kuna watu wameumia na wengine wamefaidika.

“Tunataka mikataba iwekwe juu ya meza, kwani kwa kukosa uelewa baadhi ya mabondia hukatwa fedha nyingi kwa kuwa hawana mwongozo wala wanaowapigania,” anasema Waziri Mwakyembe.

Naye promota wa mchezo huo, Shomari Kimbau, anaipongeza Serikali kwa kuonyesha nia ya dhati ya kusaidia mchezo wa masumbwi nchini.

“Lazima yawepo mazingira mazuri ya kusimamia mchezo huu, ili upendwe na watu wengine pamoja na kurudisha imani kwa wadau na wawekezaji waweze kuwekeza fedha zao.

“Hiki kinachofanywa na Serikali ni kitu kizuri na kinafaa kuungwa mkono na wadau wa mchezo huu,” anasema Kimbau.

Kwa upande wake, Rais wa Shirikisho la Ngumi za Kulipwa Tanzania (TPBO), Yassin Abdallah, anasema kinachofanywa na Serikali kitakuwa na faida kubwa, kama kweli kitatekelezwa kikamilifu.

“Serikali ndiyo kila kitu, kama imeamua kuusimamia mchezo huu huenda kukawa na mabadiliko makubwa, ikiwamo kurudisha heshima iliyopotea kwa muda mrefu,” anasema Abdallah.

Wakala na bondia wa zamani, Chaurembo Palasa, anasema kabla Dk. Mwakyembe hajaonyesha matamanio yake katika kuusaidia mchezo huo, uligubikwa na vurugu nyingi kutokana na kukosa utaratibu mzuri.

“Kwenye mchezo wowote duniani utaratibu ni jambo jema, lakini hata kama kukiwa na chama kimoja lazima watu watakaoongoza wawe na uzoefu.

“Mchezo huu ulivurugika kutokana na kuwapo na vyama vingi vya ngumi ambavyo vilikuwa vikisababisha kuwapo kwa makundi ambayo yalikuwa yakitetea maslahi binafsi,” anasema Palasa.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
591,000SubscribersSubscribe

Latest Articles