24.2 C
Dar es Salaam
Saturday, November 16, 2024

Contact us: [email protected]

Dk. Mpango aeleza uchumi ulivyo sasa

RAMADHAN HASSAN Na NORA DAMIAN-DODOMA/DAR

WAZIRI wa Fedha na Mipango, Dk. Philip Mpango, amesema uchumi wa Tanzania unaendelea kukua kwa kasi zaidi kulinganisha na nchi zingine za Jumuiya ya Afrika Mashariki na zile za SADC.

Amesema pia nchi imeingia katika vita kubwa ya kiuchumi ndani na nje ya nchi.

Akizungumza mjini Dodoma jana wakati wa kuwasilisha taarifa ya hali ya uchumi wa Taifa na utekelezaji wa Bajeti ya Serikali kwa kipindi cha Julai hadi Novemba, mwaka huu, Waziri  alisema uchumi umekua kwa wastani wa asilimia 7.1 (2017), ikilinganishwa na asilimia 7.0 kwa miaka ya 2015/2016.

“Kwa nchi za Afrika Mashariki, uchumi wa Tanzania ulikua kwa asilimia 7.1 mwaka 2017 ukilinganisha na Rwanda (6.1), Uganda (5.1), Kenya (4.9), na Burundi (0.0) na kwamba Tanzania iliongoza katika ukuaji wa uchumi hata katika nchi za SADC,” alisema Dk. Mpango.

Alisema katika kipindi cha Januari hadi Juni, pato la Taifa lilikua kwa asilimia 7.0, ikilinganishwa na asilimia 6.3 katika kipindi kama hicho mwaka 2017.

Alitaja sekta zilizokua kwa kasi zaidi na ukuaji wake katika mabano kuwa ni ujenzi (asilimia 15.7), uzalishaji viwandani (12.0), habari na mawasiliano (11.2) na uchukuzi na uhifadhi mizigo (8.2).

Alisema Tanzania imeendelea kuwa miongoni mwa nchi tano bora kwa kasi ya ukuaji wa uchumi katika Bara la Afrika katika nusu ya kwanza ya 2018, ikijumuisha na Ethiopia (8.5), Ivory Coast (7.4), Rwanda (7.2), Tanzania (7.0) na Senegal (7.0).

Alisema sekta zilizoendelea kutoa mchango mkubwa katika pato la Taifa kuanzia Januari – Juni, mwaka huu, ni kilimo (asilimia 34.5), ujenzi (16.8), biashara (10.1) na kwamba kilimo kilikua kwa asilimia 3.6 kwa kipindi hicho.

MFUMUKO WA BEI

Waziri Mpango, alisema mfumuko wa bei umeendelea kupungua kutoka wastani wa asilimia 4.3 mwaka 2017/18 hadi kufikia asilimia 3.0 Novemba 2018.

Alisema kati ya Julai hadi Novemba 2018, Tanzania ilikuwa na kiwango kidogo zaidi cha mfumuko wa bei ikilinganishwa na Uganda asilimia (3.3) na Kenya (4.8).

 “Mfumuko wa bei ya chakula ulifikia asilimia 2.0 Novemba, mwaka huu, ikilinganishwa na asilimia 7.9 katika kipindi kama hicho mwaka 2017,”alisema.

Dk.Mpango alizitaja sababu zingine kuwa ni kutengamaa kwa bei za mafuta katika soko la dunia na utekelezaji madhubuti wa sera za fedha na za bajeti.

HALI YA MAISHA YA WANANCHI

Alisema kasi kubwa ya ukuaji wa uchumi imesababisha kuimarika kwa hali ya maisha ya wananchi hasa wale waliopata fursa za ajira katika shughuli za kiuchumi zinazokua haraka, kama vile ujenzi na ukarabati wa miundombinu ya barabara, reli, upanuzi wa bandari na viwanja vya ndege.

Alisema ukuaji mzuri wa uchumi umeiwezesha Serikali kuongeza ukusanyaji wa mapato na kugharamia uboreshaji wa huduma za jamii kama ujenzi wa vituo vya afya, zahanati, madawa, vifaa tiba, vitendanishi, maji na kuimarisha uzalishaji wa umeme na kuusambaza vijijini.

“Kutokana na kiwango kidogo cha mfumuko wa bei uwezo wa shilingi kununua vitu ni mkubwa,”alisema.

THAMANI YA SHILINGI

Alisema thamani ya shilingi ya Tanzania imeendelea kuwa tulivu ambapo kuanzia Julai hadi Novemba 2018 ambapo Dola moja ya Marekani ilibadilishwa kwa wastani wa Sh 2,276, ikilinganishwa na Sh 2,235 katika kipindi cha Julai hadi Novemba, 2017.

“Hivyo, shilingi ilipungua thamani dhidi ya dola kwa asilimia 1.8,  kiwango ambacho ni kidogo na hakikuathiri utulivu wa thamani ya shilingi ya Tanzania ikizingatiwa kuwa mfumuko wa bei wa wastani katika nchi washirika wakuu wa biashara na Tanzania ni asilimia 3.0,”alisema. 

HATUA ILIZOCHUKUA

Dk. Mpango, alisema katika kipindi cha nusu ya kwanza ya mwaka 2018/19, Serikali kupitia Benki Kuu ya Tanzania (BoT), ilichukua hatua mbalimbali kuongeza ukwasi kwenye uchumi ili kuziwezesha benki za biashara kuongeza utoaji wa mikopo kwa sekta binafsi.

Alizitaja hatua hizo kuwa ni kutoa mikopo ya muda mfupi kwa mabenki, kushusha riba ya mikopo kwa mabenki kutoka asilimia 9.0 hadi asilimia 7.0 Agosti 2018 na kununua fedha za kigeni kutoka katika benki za biashara na taasisi za Serikali.

Alisema kutokana na hatua hizo, ukwasi kwenye mabenki ya biashara uliongezeka na riba katika masoko ya fedha zilipungua.

BENKI

Alisema sekta ya kibenki imeendelea kuwa imara, salama na yenye kutengeneza faida, ikiwa na mitaji na ukwasi wa kutosha zaidi ya kiwango kinachotakiwa kisheria.

“Uwiano wa mitaji ya mabenki ikilinganishwa na rasilimali zao ulikuwa asilimia 16.3, ikiwa juu ya kiwango kinachohitajika kisheria cha asilimia 10.0.

“Kiwango cha mali inayoweza kubadilishwa kuwa fedha taslimu ikilinganishwa na kiwango cha amana zinazoweza kuhitajika katika muda mfupi kilifikia asilimia 36 ikilinganishwa na kiwango cha chini kinachohitajika kisheria cha asilimia 20.

“Hii inaashiria kuwa mabenki yana ukwasi wa kutosha kwa ajili ya shughuli zake za kila siku ikiwemo kulipa madeni pamoja na kutoa mikopo,”alisema.

MADUKA YA FEDHA

Alisema Serikali kupitia BoT imeendelea kuchukua hatua za kuimarisha biashara ya maduka hayo kuondoa uwezekano wa kufanya biashara isiyo halali ambayo ni pamoja na utakatishaji wa fedha haramu.

Dk. Mpango alisema hatua zilizochukuliwa ni pamoja na BoT kufanya msako wa kukagua maduka hayo jijini Arusha na kubaini baadhi ya mambo ambayo yalikuwa yanafanywa kinyume na leseni zao.

“Zoezi hili litakuwa endelevu ili kuhakikisha kwamba mwenendo wa maduka haya unaridhisha,”alisema.

MAPATO YA SERIKALI

Kuanzia Julai hadi Novemba mwaka huu, makusanyo ya ndani (ikijumuisha mapato ya Halmashauri) yalifikia Sh trilioni 7.37 sawa na asilimia 88.9 ya makadirio ya Sh trilioni 8.30 katika kipindi hicho.

Dk. Mpango alisema mapato ya kodi yalifikia Sh trilioni 6.23 ikiwa ni sawa na asilimia 88 ya lengo la kukusanya Sh trilioni 7.04 kwa kipindi hicho.

DENI LA SERIKALI

Dk. Mpango alisema hadi kufikia Septemba mwaka huu deni la Serikali lilifikia Sh trilioni 49.37 sawa na ongezeko la asilimia 3.2 ikilinganishwa na Sh trilioni  47.82 Septemba mwaka jana.

Alisema deni la ndani lilikuwa Sh trilioni 13.64 sawa na asilimia 27.6 huku la nje likiwa ni Sh trilioni 35.72 sawa na asilimia 72.4.

MATARAJIO 2019

Alisema uchumi unatarajiwa kuendelea kukua kutokana na uwekezaji mkubwa unaoendelea kwenye miundombinu wezeshi ya uzalishaji mali kama vile barabara, madaraja, bomba la mafuta, ujenzi wa reli kwa kiwango cha kimataifa na viwanja vya ndege.

Alisema ujenzi wa kituo cha kufua umeme utokanao na nguvu za maji katika mto Rufiji chenye uwezo wa kuzalisha megawati 2,100 kwa ajili ya matumizi ya majumbani na viwandani na maboresho katika sekta ya madini na kilimo na uanzishwaji wa kanda maalum za kiuchumi (EPZ/SEZ).

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
591,000SubscribersSubscribe

Latest Articles