Na Mwandishi Wetu, Dodoma
Licha ya matibabu ya magonjwa yasiyoambukiza kuwa na gharama kubwa na yana hitaji tiba wakati wote, Serikali imekuwa ikitoa msamaha wa matibabu kwa wagonjwa wanaougua magonjwa yasiyoambukiza ambao wamethibitika kuwa hawana uwezo wa kugharamia matibabu yao kwa mujibu wa Sera ya Afya.
Hayo yamesemwa leo Alhamisi Juni 9, 2022 na Naibu Waziri wa Afya, Dk. Godwin Mollel alipokuwa akijibu swali lililoulizwa na Mbunge wa Jimbo la Chaani, Juma Usonge Hamad aliyehoji Serikali ina mpango gani wa kutoa matibabu bure kwa maradhi yasiyoambukiza kama Kisukari, Presha na Shinikizo la Damu.
Hata hivyo, Dk. Mollel amesema kuwa Serikali ipo katika hatua za mwisho za ukamilishaji wa Muswada wa Bima ya Afya kwa Wote ambao utawezesha wananchi wote kupata huduma za afya katika vituo vyote vya kutolea huduma za afya nchini.
Akijibu swali la nyongeza lilioulizwa na Mheshimiwa Usonge aliyehoji usumbufu wanaopata wazee pindi wanapoenda hospitalini kupata huduma za matibabu, Dk. Mollel ameendelea kuwasisitiza wataalam kufuata maagizo yanayotolewa na viongozi ikiwemo kuhakikisha Wazee wanapata matibabu bure katika vituo vya kutolea huduma za afya.
“Nitumie fursa hii kutoa agizo kwa Waganga wote wa Mikoa na Wilaya, suala la matibabu kwa wazee ni bure na wanatakiwa kuwa na dirisha lao la kupata huduma, hatutegemei kusikia tena malalamiko ya wazee wanapitia mlolongo mrefu wa kupata huduma za matibabu,” amesisitiza Dk. Mollel.