25.9 C
Dar es Salaam
Thursday, December 19, 2024

Contact us: [email protected]

DK. MOKIWA ALIPASUA KANISA LA ANGLIKANA

Dk. Valentine Mokiwa
Dk. Valentine Mokiwa

Na ASHA BANI – Dar es Salaam

HATUA ya walei 32 wa Kanisa la Anglikana Dayosisi ya Dar es Salaam kumfungulia Dk. Valentine Mokiwa mashtaka 10, yakiwamo ya ufisadi wa mali za kanisa, ambayo yamemvua Uaskofu Mkuu wa Dayosisi ya Dar es Salaam, inaonekana kutishia kulipasua kanisa hilo vipande viwili.

Pamoja na Askofu Mkuu wa Kanisa la Anglikana Tanzania, Dk. Jacob Chimeledya kubariki hatua hiyo kumvua uaskofu, kiongozi huyo amekutana na mapadri wa kanisa hilo katika kikao cha siri kilichofanyika Kanisa la Anglikana Ilala, Dar es Salaam jana.

Katika kikao hicho, Askofu Mokiwa amewashawishi mapadri wa dayosisi hiyo kusaini fomu maalumu ya kupinga uamuzi huo wa kanisa wa kumvua madaraka na uaskofu.

Pamoja na hayo, Askofu Mokiwa amevunja pia Baraza la Halmashauri ya Kudumu na kuchagua wajumbe wengine 10 ili kuunda baraza jipya.

Akizungumza na MTANZANIA kwa simu jana, Katibu Mkuu wa Makanisa ya Anglikana Tanzania, Mchungaji Johnson Chinyong’ole alisema pamoja na kiongozi huyo wa zamani kuendelea na vikao vyake, lakini bado kanisa litaendelea kusimamia msimamo wake.

“Tamko la kuondolewa kwake ameshajulishwa kitambo na kuwa hana cheo, unapoambiwa huna uaskofu wa Dayosisi, hivyo wewe ujue huna tu basi ukae pembeni.

“Yani ni kama vile mabadiliko katika nchi yakitokea ya kumwondoa rais, haiwezekani akarudishwa tena, hivyo ametolewa ajue ametolewa,’’ alisema Mchungaji Chinyong’ole.

Naye Mkuu wa Kanisa la Mtakatifu Andrea lililopo Magomeni, Dar es Salaam, Sylivester Haule ambaye alikuwa ndiye mwenyekiti na msemaji wa tume iliyoundwa kumchunguza Mokiwa, alisema hayo huenda ni makeke yake mwenyewe na staili ya jinsi alivyoamua kuondoka.

“Kwa kuwa alikuwa maarufu, hivyo kuondoka kwake ni shida, lakini mbona yeye aliwahi kuwaondosha viongozi waliokosea na hawakubisha wala kugoma?’’ alisema Haule.

Mokiwa ambaye hadi anastaafishwa kwa lazima alikuwa Askofu Mkuu wa Kanisa la Anglikana Dayosisi ya Dar es Salaam.

Uamuzi wa kumvua uskofu ulifanywa juzi na Askofu Chimeledya baada ya Askofu Mokiwa kugoma kujiuzulu kama ilivyoshauriwa na nyumba ya maaskofu ambayo ilimkuta na hatia ya kufuja mali za kanisa hilo na kukiuka maadili ya kichungaji ambayo yalibainishwa kwenye ripoti ya uchunguzi iliyoundwa na kiongozi mkuu wa kanisa hilo nchini.

Taarifa za ndani ya kanisa hilo zilieleza kuwa katika kikao kilichofanyika kanisani Ilala, Askofu Chimeledya na timu yake walihudhuria kikao cha halmashauri ya kudumu ya Dayosisi ya Dar es Salaam, akatangaza uamuzi wa kumvua uaskofu Dk. Mokiwa chini ya ulinzi wa polisi.

Pamoja na uamuzi huo, Dk. Chimeledya pia aliagiza waraka huo wa kuondolewa madarakani kwa askofu huyo usambazwe katika makanisa yote yaliyoko chini ya Dayosisi ya Dar es Salaam na usomwe kwenye ibada mbele ya waumini juzi Jumapili.

Akizungumza na gazeti moja la kila siku (Si MTANZANIA) juzi, Katibu Mkuu wa Dayosisi ya Dar es Salaam, Padri Jonathan Senyagwa, alikanusha taarifa na barua ambazo zimesomwa katika baadhi ya makanisa jijini Dar es Salaam zilisomwa kwa makosa.

“Mwenye mamlaka ya kumfukuza kazi ni yule aliyemwajiri, na mwajiri wa Dk. Mokiwa ni Sinodi ya Dar es Salaam… tutatoa tamko hivi karibuni kuthibitisha kwamba askofu wa jimbo bado hajafukuzwa,” alisema Padri Senyagwa wakati akizungumza na gazeti hilo.

Hata hivyo, aliupinga waraka uliosambzwa na Askofu Mkuu wa Tanzania na kudai kwamba haujapitia kwenye halmashauri ya kudumu ya dayosisi ili kupata baraka zake.

Alisema halmashauri iligoma kubariki uamuzi huo kwa sababu Kanisa la Anglikana Tanzania lina kanuni na taratibu zake.

Juzi, mwenyekiti huyo wa Tume ya Uchunguzi alisema kuwa eneo jingine ambalo liliingia katika kosa namba tatu ni la Benki ya Wananchi Dar es Salaam (DCB), ambayo makubaliano ya awali wawekezaji hao walitakiwa kufanya ujenzi kulipa Sh bilioni 5 kisha kuwa mali ya kanisa, lakini Mokiwa aliandikisha kwa Sh bilioni mbili na baada ya mkataba kuisha aliwatetea wawekezaji hao.

“Unajua ilikuwa ni kama aina fulani ya ufisadi, maana makubaliano na waliojenga ilikuwa walipe Sh bilioni 5, walivyotugeuka Askofu Mokiwa anatetea naye na kusema kuwa ni Sh bilioni 2 jambo ambalo si sahihi,’’ alisema.

Aliongeza kuwa baada ya kukaidi, maaskofu wakuu walikutana kujadili suala hilo kuanzia Desemba 21 hadi 24 na baada ya hapo maamuzi yakatolewa Januari 7 kwa kuamua kuwa si askofu tena.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
592,000SubscribersSubscribe

Latest Articles