28.2 C
Dar es Salaam
Friday, November 15, 2024

Contact us: [email protected]

Dk. Makongoro Mahanga hatunaye

Andrew Msechu -Dar es salaam

MWENYEKITI wa Chadema Mkoa wa kichama wa Ilala, ambaye pia ni Mjumbe wa Kamati ya Utendaji Kanda ya Pwani, Dk. Makongoro Mahanga amefariki dunia jana wakati akitibiwa Hospitali ya Taifa ya Muhimbili.

Akithibitisha taarifa za kifo hicho jana, Ofisa Habari na Mawasiliano wa Chadema Kanda ya Pwani, Gerva Lyenda alisema Dk. Mahanga alifikwa na mauti jana saa 12.30 asubuhi akiwa anatibiwa Hospitali ya Taifa Muhimbili alikolazwa tangu Jumamosi iliyopita.

Lyenda alisema kutokana na msiba huo, mipango yote ya maziko inafanyika nyumbani kwake Tabata Segerea.

“Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema) Kanda ya Pwani kinasikitika kuutangazia umma kuwa Mjumbe wa Kamati ya Utendaji Kanda ambaye pia ni Mwenyekiti wa Chadema Mkoa wa Ilala, Dk. Makongoro Milton Mahanga amefariki dunia.

“Katibu wa Chadema Kanda ya Pwani, Hemed Alli anawaomba wanachama wote kukusanya michango ya rambirambi kwa wahazini wa majimbo yao ambao wataiwakilisha kwa Ofisa Fedha na Rasilimali wa Kanda, Jerry Kerenge,” alisema Lyenda.

ACT WAOMBOLEZA

Chama cha ACT Wazalendo kilieleza jana kuwa kimepokea kwa mshtuko na masikitiko makubwa taarifa ya kifo cha Dk. Mahanga.

Taarifa iliyotolewa na Naibu Katibu wa Idara ya Habari, Uenezi na Mahusiano kwa Umma, Janeth Rithe jana, ilisema Dk. Mahanga ni mwanasiasa mkongwe ambaye amewahi pia kuwa Mbunge wa Ukonga (baadaye Segerea baada ya Ukonga kugawanywa) na Naibu Waziri wa Kazi na Ajira.

“ACT Wazalendo tunaipa pole familia ya Dk. Mahanga, uongozi wa Chadema wa Mkoa wa kichama wa Ilala, Kanda ya Pwani na Taifa kwa msiba mkubwa uliowakuta. ACT Wazalendo tupo pamoja nao katika kipindi hiki kigumu cha kumpoteza mpendwa wao,” alisema Janeth.

Alisema ACT Wazalendo wanamwomba Mwenyezi Mungu ailaze roho ya Dk. Mahanga mahali pema.

Dk. Mahanga amewahi kushika nyadhifa mbalimbali serikalini ikiwemo Naibu Waziri wa Kazi na Ajira hadi Agosti 2, 2015 alipotangaza rasmi kujivua uanachama wa CCM na kujiunga na Chadema, siku moja baada ya kudai kutotendewa haki katika mchakato wa kura za maoni.

WASIFU WAKE

Dk. Mahanga ni mwanasiasa ambaye amekuwa Mbunge wa Ukonga kupitia CCM na baadaye Segerea kwa jumla ya miaka 14 kuanzia mwaka 2000, na Naibu Waziri wa Miundombinu na baadaye Kazi na Ajira kwa jumla ya miaka tisa kuanzia mwaka 2006.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
591,000SubscribersSubscribe

Latest Articles