AZIZA MASOUD- DAR ES SALAAM
SERIKALI imewataka wanadiplomasia wajipange kwa lengo la kulifikisha taifa katika uchumi wa kati ifikapo mwaka 2025.
Kauli hiyo imetolewa juzi Dar es Salaam na Waziri wa Mamboya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa, Balozi Augustine Mahiga wakati wa mahafali ya 21 ya Chuo cha Diplomasia Kurasini.
Alisema Serikali inahitaji mafanikio kupitia diplomasia ya uchumi ndani ya awamu ya tano, tofauti na ilivyokuwa katika awamu nyingine ambapo ilikuwa na msimamo wa diplomasia ya jumla.
“Kipindi hiki cha awamu ya tano kimeitwa ni kipindi cha ‘transformation’ (mabadiliko), ningependa chuo hiki kama vile vyuo vingine tuelewe dhamira na mwelekeo wa hayo mabadiliko ambayo Rais wetu Dk. John Magufuli anataka yafanyike.
“Hii diplomasia ya uchumi tunataka ituletee mafanikio, na mahali pa kuanzia ni hapa chuoni, wahusika lazima tuangalie katika mitaala tunawafundisha nini ili wawe wanadipolomasia wa kutuletea uchumi wa viwanda,” alisema Dk. Mahiga.
Alisema maprofesa waliopo chuoni hapo wanapaswa kuwaelewesha wanafunzi kuhusu faida za uchumi wa viwanda nchini.
Dk. Mahiga alisema katika diplomasia ya uchumi wa viwanda, kitu kikubwa kinachopaswa kufanywa ni kushawishi na kuleta wawekezaji kuanzisha viwanda, mitaji ya moja kwa moja au ubia.
“Lazima tutafute mitaji ndani na nje ya nchi, huwezi kuwa na viwanda bila kuwa na wawekezaji, huwezi kuandisha viwanda bila kuwa na nishati, hivyo wanadiplomasia wangu lazima mjue ni nani anaweza kutupatia nishati ya kudumu ya kuhudumia viwanda na kuanza kumshawishi,” alisema.
Alisema viwanda vinavyotakiwa kujengwa nchini vinapaswa vitokane na rasilimali za nchi kama wanavyofanya nchi nyingine akitolea mfano Japan na Uingereza.
Aidha aliwataka viongozi wa chuo hicho kuanzisha mtaala wa diplomasia ya mtandao ambayo itasaidia kuitangaza Tanzania duniani.
“Kitu kinachoendelea kwa sasa ni mitandao, nataka chuo kifundishe ‘cybe’ diplomasia, maana yake sio tu kubonyeza bonyeza na kuangalia internet, tunataka tuinadi Tanzania.
“Wizara yangu ama ile ya Utalii hatutaweza kuitangaza nchi duniani, nataka tuwe na diplomasia ambayo ‘uki-tweet’ kwa dakika mbili unaiona Tanzania, hilo ndilo somo ninalolitaka kwa sasa la kuinadi Tanzania yetu,” alisema.
Kwa upande wake KaimuMkuu wa chuo hicho, Dk. Bernald Achiula, alisema chuo kina mpango mkakati wa kuongeza idadi ya udahili kwa wanafunzi, kuboresha ufundishaji, utafiti na kutoa ushauri kwa wataalamu, kukitangaza ndani na nje ya nchi, kujenga mahusiano na vyuo vingine na kuboresha miundombinu.
Aidha, alisema chuo hicho ni pekee kinachotoa elimu ya diplomasia ya uchumi ili kuisaidia Serikali ya Awamu ya Tano katika sera yake ya kuifanya Tanzania kufikia uchumi wa kati ifikapo mwaka 2025.
Naye Mwenyekiti wa bodi ya chuo hicho, Balozi Ombeni Sefue, alisema chuo hicho kimefurahishwa kupatiwa bajeti ya maendeleo ya Sh bilioni 2 ambayo itakwenda kufanya ukarabati wa chuo na kukifanya kiwe cha kisasa.
Alisema mchakato wa kumpata mkandarasi kwa ukarabati wa chuo hicho unaendelea na wanatarajia kuanza ujenzi wa majengo ya kisasa kuanzia Machi.
Katika mahafali hayo, wahitimu 446 walitunukiwa vyeti katika ngazi za cheti, stashahada, shahada pamoja na shahada ya uzamili ya menejimenti ya mahusiano ya kimataifa na diplomasia ya uchumi