30.3 C
Dar es Salaam
Tuesday, December 7, 2021

Wazazi wapelekeni mapema hospitali watoto wenye jinsia mbili

MOJA ya habari iliyowahi kuandikwa na gazeti hili ilikuwa ni taarifa ya Bingwa wa Upasuaji wa Hospitali ya Taifa Muhimbili (MNH), Dk. Zaitun Bokhari, iliyosema tatizo la watoto wanaozaliwa na jinsia tata au jinsia mbili linaongezeka nchini.

Dk. Bokhari aliliambia gazeti hili katika mahojiano yake maalumu kuwa
tatizo hilo linajulikana kitaalamu kama Ambiguous Genitalia, ikiwa ni neno linalotumika kuelezea viungo vya siri vya mtoto aliyezaliwa, ambavyo ni vigumu kujua kama ni wa kike au kiume.

Kwamba kutokana na mkanganyiko, Dk. Bokhari alisema wazazi wengi hawana uelewa wa kutosha kutambua mapema tatizo hilo na kudhani ni hali ya kawaida.

Licha ya kwamba MNH inatoa matibabu ya kibingwa, lakini bado Dk. Bokhari anasema waliofikishwa hospitalini hapo walikuwa wamechelewa kwa maana ya kufikia umri mkubwa kuanzia miaka mitatu hadi 29 huku kwa mwezi hupokea kati ya watoto watano hadi sita wanaokabiliwa na tatizo hilo.

Kutokana na changamoto hiyo, sisi wa MTANZANIA Jumapili tunawaomba wazazi kuwa makini na kuchunguza ukuaji na maumbile ya mtoto.

Kama ambavyo mtaalamu huyo bingwa alivyoeleza, kwamba yapo matibabu ya tatizo hilo kwa maana ya upasuaji ambao hutolewa baada ya makubaliano kwa mujibu wa sheria, pia wazazi wanapaswa kuligundua mapema kwa kuwa si jambo la kawaida ili kuweza kupata ufumbuzi ikiwamo kuwashirikisha wataalamu wa afya ili kuchunguza zaidi.

Tunasema hivyo kwa sababu tatizo hilo likigunduliwa mapema tangu mtoto akiwa mdogo hata kama hatofanyiwa upasuaji itamsaidia mzazi au mlezi kumlea mwanaye kwa jinsia ambayo ina nguvu katika maumbile ya mwili wake.

Tunaamini kuwa tatizo hilo likigunduliwa mapema hata unyanyapaa utapungua kwa kuwa mtoto tayari anakuwa anajua ana jinsia tata tangu akiwa mdogo.

Pia wazazi au walezi wenye watoto wenye tatizo hilo, hasa wale ambao wana umri mkubwa, wanapaswa kushirikiana na kuwa karibu na watoto ili kuondoa kutojiamini pamoja na kuwafanya waweze kujiona wako sawa na watoto wengine.

Pia jamii inayogundua mtoto mwenye tatizo hilo inapaswa kuwa karibu naye kwa kumtia moyo na si kuongoza kumsema na kumcheka kwa sababu kitendo hicho kitamfanya ajione kuwa ni mwenye kasoro kubwa.

Tunatarajia mwitikio zaidi kwa wazazi au walezi kuwagundua watoto wao wenye tatizo hilo na kuwafikisha hospitali ili waweze kupatiwa ufumbuzi.

- Advertisement -
bestbettingafrica

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

66,457FansLike
168,424FollowersFollow
527,000SubscribersSubscribe
- Advertisement -
10Bet

Latest Articles