Na Kulwa Mzee, Dar es Salaam
NAIBU Waziri wa Kazi, Ajira na Maendeleo ya Vijana, Dk. Makongoro Mahanga, ameshindwa kufika mahakamani kuthibitisha kwamba kashfa ya kughushi vyeti ilikuwa ya uongo.
Hayo yamebainika baada ya Mahakama Kuu Kanda ya Dar es Salaam, kuifuta kesi ya madai ya kashfa ya kughushi vyeti iliyokuwa imefunguliwa na Dk. Mahanga dhidi ya Mwanaharakati, Kainerugaba Msemakweli na wenzake.
Kesi hiyo ilifutwa jana na mahakama hiyo kutokana na kile kilichoelezwa kuwa Dk. Mahanga alishindwa kutokea siku ya kesi yake.
Dk. Mahanga alifungua kesi hiyo ya madai namba 145/2009 dhidi ya Mwanaharakati, Kainerugaba Msemakweli na wenzake kwa madai kuwa walimtuhumu kuwa ameghushi vyeti vya elimu.
Mbali na Msemakweli wadaiwa wengine ni Mwandishi wa Gazeti la Nipashe, Muhibu Saidi, Mhariri Mtendaji wa gazeti hilo na Kampuni ya The Guardian Limited waliokuwa wanatetewa na Wakili wa kujitegemea, Michael Ngaro.
Uamuzi huo ulitolewa na Jaji Salvatory Bongole ambaye alisema amefikia uamuzi huo kwa sababu Wakili wa mlalamikaji, Kennedy Fungamtama na mlalamikaji wamekuwa hawafiki mahakamani bila kutoa taarifa na kwamba kuna ushahidi unaonyesha wito wa kuitwa mahakamani ulikuwa ukiwafikia kwa wakati.
Jaji Bongole alisema ametumia amri ya tisa kanuni ya nane ya Sheria ya Madai ya mwaka 2002 na kwamba ameifuta kesi hiyo kwa gharama.
Kwa mujibu wa hati ya madai, Dk. Mahanga alikuwa akiomba wadaiwa wamlipe Sh bilioni tatu ambazo ni fidia ya madhara aliyoyapata kutokana na habari ya uongo iliyochapishwa na wadaiwa katika Gazeti la Nipashe la Oktoba 19, mwaka 2009 iliyokuwa na kichwa cha habari kisemacho, ‘Vyeti vya Elimu: Mawaziri sita wanasa’.