26.3 C
Dar es Salaam
Thursday, November 28, 2024

Contact us: [email protected]

DK. KINGWANGALLA ASIMULIA ALIVYONUSURIKA AJALINI

 

*Asema ilikuwa mbaya, amshukuru Mungu

*Ofisa Habari Maliasili azikwa nyumbani kwao Hai

Na TUNU NASSSOR, DAR ES SALAAM


SIKU moja baada ya kutokea kwa ajali ya gari iliyomjeruhi Waziri wa Maliasili na Utalii, Dk. Hamis Kingwangalla na maofisa wake, hatimaye kiongozi huyo amesimulia namna alivyosurika huku Ofisa habari wake, Hamza Temba akipoteza maisha.

Akizungumza jana baada ya kutembelewa na Waziri Mkuu Kassim Majaliwa, Dk. Kingwangalla, alisema anamshukuru Mwenyezi Mungu kwa sababu ajali ilikuwa mbaya sana.

Waziri huyo alipata ajali juzi asubuhi katikati ya vijiji vya Mdolii na Minjingu Wilaya ya Babati mkoani Manyara baada ya gari lake kupinduka na kusababisha kifo cha Ofisa Habari wa Wizara ya Maliasili na Utalii, Hamza Temba na wengine kujeruhiwa.

Akizungumza jana baada ya Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa kumtembelea na kumpa pole, Dk. Kigwangalla alisema ajali hiyo ilikuwa mbaya na anamshukuru Mungu.

“Ajali ilikuwa mbaya sana, hivi sasa naongea hapa namshukuru Mungu, Serikali pamoja na madaktari na wauguzi kwa jitihada kubwa walizozifanya,” alisema Dk. Kigwangalla.

Naye Waziri Mkuu ambaye aliambatana na mkewe Mary Majaliwa, alisema amefarijika baada ya kumkuta Dk. Kigwangalla na wagonjwa wengine waliolazwa katika hospitali hiyo wakihudumiwa vizuri.

“Hospitali ya Muhimbili ndio kimbilio letu kwa sasa na tunawashukuru madaktari na wauguzi kwa kazi nzuri mnayoifanya ambayo inaliletea heshima Taifa letu kwani hata watu wa Comoro wanakuja kutibiwa Muhimbili,” alisema Majaliwa.

Naye Meneja Mawasiliano wa Hospitali ya Taifa Muhimbili (MNH), Aminiel Eligaesha, alisema afya ya waziri huyo imeanza kuimarika.

“Hali ya Dk. Kigwangallah inaimarika kwa sasa baada ya kupatiwa matibabu hospitalini hapa,” alisema Eligaesha.

Alisema Dk. Kigwangala alipokewa juzi na kulazwa katika wodi ya Mwaisela na kuanza kupatiwa matibabu.

Baada ya kutokea kwa ajali hiyo Dk. Kigwangalla na wasaidizi wake walipelekwa kituo cha afya cha Magugu na baadaye kuhamishiwa hospitali ya Selian jijini Arusha kisha hospitalini hapo.

Kwa mujibu wa Kamanda wa Polisi wa Manyara, Augustino Senga, chanzo cha ajali  hiyo ni mwendo kasi wa dereva na alipokuwa akijaribu kumkwepa Twiga aliyeingia barabarani ghafla katika eneo la Jumuiya ya Hifadhi ya Jamii ya Burunge inayopakana na na hifadhi ya Tarangire na Manyara.

Akiwa hospitalini hapo Waziri Mkuu alimjulia hali msanii maarufu wa maigizo nchini, Amri Athumani maarufu King Majuto, ambaye amelazwa hospitalini hapo akipatiwa matibabu na kusema amefarijika kumkuta akiwa anaendelea vizuri.

Naye Mzee Majuto aliishukuru Serikali kwa sababu inamuhudumia vizuri.

“Mheshimiwa nakushukuru sana na naishukuru Serikali kwani hata sijui ingekuwaje kama si msaada wa Serikali. Hii ni bahati kubwa,” alisema Majuto.

Pia Waziri Mkuu alimjulia hali Hellena Baruti ambaye ni mama mzazi wa Mthamini Mkuu wa Serikali, Evelyne Mugasha, aliyelazwa katika Taasisi ya Moyo ya Jakaya Kikwete (JKCI) akipatiwa matibabu.

Temba azikwa Masama

Naye aliyekuwa Ofisa Habari wa Wizara ya Maliasili na Utalii, Hamza Temba, amezikwa jana nyumbani kwao Wilayani Hai, Tarafa ya  Masama Kijiji cha Mudio .

Mwili wa Temba, uliwasili nyumbani kwao mchana wa jana ukitokea Hospitali ya Boma Ng’ombe na kusomewa dua kwa mujibu wa taratibu za dini ya kiislamu naisha kuzikwa kwenye makaburi ya familia yaliyopo nyumbani kwao Masama.

Viongozi mbalimbali wa serikali walidhuhuria msiba huo akiongozwa na Mkuu wa Mkoa wa Kilimanjaro, Anna Mghwira, Mkuu wa Wilaya ya Hai, Lengai ole Sabaya huku Wizara ya Maliasili na Utalii, ikiongozwa na Naibu Katibu Mkuu, Dk. Aloyce Nzuki.

 

 

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
591,000SubscribersSubscribe

Latest Articles