MWANDISHI WETU -GEITA
WAZIRI wa Nishati, Dk. Medard Kalemani amewaambia wanakijiji ambao umeme ushafika katika maeneo yao walipie gharama za kuwashiwa umeme ili kufahamu idadi ya wateja, nguzo zisambazwe na kuunganishwa kulingana na wateja waliopo kwa wakati husika.
Dk. Kalemani alisema hayo wakati akiwasha umeme katika Kijiji cha Rusungwa Kata ya Nyamirembe, Wilayani Chato na Kijiji cha Businda Wilayani Bukombe mkoani Geita alipofanya ziara ya kukagua maendeleo ya usambazaji umeme vijijini katika maeneo hayo.
Alisema kuwa vijiji vingi tayari vimefikiwa na umeme katika maeneo machache hivyo wananchi wanatakiwa kulipia gharama za kuwashiwa umeme ili ifahamike idadi ya wateja waliopo na kupelekewa nguzo za kusambazwa kwa wateja waliopo na wawashiwe umeme.
Pamoja na hali hiyo alisema kuwa kitendo cha wanakijiji kuacha kulipia gharama za kuuwashiwa umeme wakisubiri kuona nguzo zimesambaa katika maeneo yao, hali ya kuwa tayari umeme umeshafika katika vijiji vyao, kunachelewesha kasi ya kuwawashia umeme wanakijiji katika nyumba zao kwa kuwa mamlaka husika zinasambaza nguzo kulingana na wateja waliopo eneo husika kwa wakati husika, hivyo wananchi wachangamkie fursa na kulipia gharama ya Sh 27,000 tu.
Hata hivyo alisema kuwa wanakijiji hao hawapaswi kuhoji kuhusu nguzo kufika katika maeneo yao kwakuwa hilo si jukumu lao, ila wanachotakiwa kufanya ni kulipia gharama za kuwashiwa umeme tu, na baada ya kulipia gharama ndipo wahoji endapo hawajawashiwa umeme.
“Kijiji chochote ambacho umeme umeshafika na kuunganishwa, hata kama umewashwa katika nyumba moja, wanakijiji sasa jukumu lenu ni kulipia gharama kuwashiwa umeme ili ijulikane idadi ya wateja waliopo na mletewe nguzo na kuungwa, nguzo zinaletwa na kusambazwa kulingana na idadi ya wateja waliopo.
“Kwa wakati husika ili wote wanaotaka kwa wakati huo wapate, msihoji kuwa nguzo zinafika lini hilo si jukumu lenu! Ninyi mnapaswa kuhoji lini mtawashiwa umeme mkiwa tayari mmelipia gharama, na hapo tutachukua hatua kwa yeyote atakayechelewa kumuwashia umeme mteja aliyekwisha lipia gharama za uunganishaji, sasa lipieni msisubiri nguzo,” alisema Dk. Kalemani
Aidha Dk.Kalemani alirejea kusema kuwa mkandarasi yeyote atakayeshindwa kumaliza kazi ya usambazaji wa umeme vijijini kwa mujibu wa mkataba,atashitakiwa kisheria kwa kosa la kuwacheleweshea wananchi huduma pamoja na kukatwa asilimia 10 ya malipo yake yaliyosalia.
Aidha kazi hiyo atapewa mkandarasi mwingine amalizie na hiyo asilimia 10 iliyokatwa ndiyo itatumika kumlipa mkandarasi atakayekabidhiwa jukumu la kumalizia kazi hiyo.