Na Mwandishi Wetu, Mwanza
Waziri wa Afya Maendeleo ya Jamii Jinsia Wazee na Watoto, Dk. Dorothy Gwajima Ameagiza Wakuu wa Mikoa, Wilaya kote nchini kuanzishwa kwa daftari la ufuatiliaji wa utekelezaji kazi za miradi ya afya ili kuonesha maendeleo na mwenendo wa kazi zinazofanyika kila siku kuepuka watekelezaji kutotimiza wajibu wao bila sababu za msingi jambo linalorudisha nyuma Kasi ya utekelezaji.
Agizo hilo amelitoa jijini Mwanza wakati akikagua ujenzi wa jengo la mama na mtoto katika hospitali ya mkoa wa Mwanza Sekou Toure linalojengwa kwa gharama ya Sh Bilioni 10 na milioni 106 kwa lengo la kupunguza msongamano wa wagonjwa hasa wakina mama wajawazito.
Dk. Dorothy Gwajima Amesema kuwa, serikali imetoa fedha nyingi kuboresha huduma za afya hivyo haitakiwa busara kuona Kasi ya utekelezaji inakuwa ndogo bila sababu za msingi.
Amesema kuwa kila mradi unaotekelezwa uwe na daftari la ufuatiliaji kwani kumbukumbu zake za taarifa ya utekelezaji uliofanywa siku hiyo zitasaidia kuonyesha mwenendo wa Kasi ya utekelezaji na maeneo yanayokwamisha ili yaweze kufanyiwa kazi kwa wakati.
Mkuu wa wilaya ya Nyamagana Amina Makilagi akimuwakilisha mkuu wa mkoa wa Mwanza, Mhandisi Robert Gabriel amesema kuwa utekelezaji wa maagizo hayo utaanza mara moja kwa kuweka wataalamu wa kufuatilia miradi ya ujenzi inayotekelezwa pamoja na kuweka madaftari kwenye miradi husika kwa lengo la kuharakisha utekelezaji na kuwabaini baadhi ya watendaji wazembe kwa kuwa daftari litaonyesha kila idara kazi iliyotekelezwa kila siku.
Kwa upande wake mganga mkuu wa mkoa wa Mwanza, Dk. Thonas Rutashunzibwa ameahidi kumsimamia kikamilifu mkandarasi TBA anayejenga jengo la Mama na mtoto katika Hospitali ya Mkoa wa Mwanza Sekou Toure ambalo utekelezaji wake umefimia asilimia 85 na ifikapo 31 Desemba 2021 mradi huo utakamilika