26.1 C
Dar es Salaam
Sunday, November 17, 2024

Contact us: [email protected]

Dk. Biteko: Bilioni 9 zimetumika kufikisha umeme wa REA katika vijiji vyote Wanging’ombe

Na Veronica Simba – REA

Naibu Waziri Mkuu na Waziri wa Nishati, Dk. Doto Mashaka Biteko ameeleza kuwa vijiji vyote 108 vya Wilaya ya Wanging’ombe mkoani Njombe vimekwishafikishiwa nishati ya umeme kupitia miradi inayotekelezwa na Wakala wa Nishati Vijijini (REA).

Aidha, amesema kuwa katika Wilaya hiyo peke yake, Serikali imetumia Sh bilioni 9.5 kupeleka umeme.

“Tunapeleka umeme katika vitongoji vyote vilivyobaki, ili watu wote wapate umeme,” ameongeza Dk. Biteko wakati akizungumza na wananchi wa kijiji cha Ikwavila wilayani humo, mapema leo, Februari 21, katika hafla ya kuwasha umeme katika Shule ya Msingi Ikwavila.

Mojawapo ya vyumba vya madarasa katika Shule ya Msingi Ikwavila, wilayani Wanging’ombe, Mkoa wa Njombe kikiwa kimeandaliwa tayari kuwashiwa umeme na Naibu Waziri Mkuu na Waziri wa Nishati, Dk. Doto Mashaka Biteko katika hafla iliyofanyika Februari 21, 2024.

Naye Mbunge wa Wanging’ombe ambaye pia ni Naibu Waziri, Ofisi ya Rais, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (TAMISEMI), Festo Dugange, amekiri na kuipongeza Serikali kupitia Wizara ya Nishati na REA kwa kuvifikishia umeme vijiji vyote 108 vya Wilaya hiyo.

“Mheshimiwa Naibu Waziri Mkuu na Waziri wa Nishati, kati ya vitongoji 525 tulivyonavyo, watendaji wako wachapakazi tayari wametuletea umeme katika vitongoji 295,” amesema.

Naibu Waziri Mkuu na Waziri wa Nishati, Dk. Doto Mashaka Biteko akizungumza kabla ya kuwasha umeme katika Shule ya Msingi iliyopo kijiji cha Ikwavila, Wilaya ya Wanging’ombe, Mkoa wa Njombe, Februari 21, 2024.

Akieleza zaidi, Dugange amesema kuwa katika Mwaka huu wa Fedha, Serikali imeanza utekelezaji wa miradi ya REA katika vitongoji vingine 72 huku vitongoji 158 vilivyobaki vikiwa na wakandarasi ambao wanaendelea na kazi.

Akiwasilisha taarifa ya utekelezaji wa miradi ya umeme vijijini, Mwakilishi wa Mkurugenzi Mkuu wa REA, Mhandisi Godfrey Chibulunje ameeleza kuwa kwa sasa REA inatekeleza jumla ya miradi mitatu katika maeneo tofauti ya Wilaya ya Wanging’ombe.

Ameitaja miradi hiyo kuwa ni pamoja na REA Awamu ya Tatu Mzunguko wa Pili, Mradi wa Ujazilizi Fungu la Pili B pamoja na Mradi wa kupeleka umeme kwenye Vituo vya Afya na Pampu za Maji.

Kuhusu takwimu za Mkoa wa Njombe, ameeleza kuwa jumla ya vijiji 361 kati ya 381 vimekwishafikishiwa umeme wa REA, sawa na asilimia 94.75.

Aidha, vitongoji 1,148 kati ya 1,836 sawa na asilimia 62.5 tayari vimefikiwa na umeme kupitia miradi mbalimbali ya REA.

Sehemu ya Umati wa Wananchi wakimsikiliza Naibu Waziri Mkuu na Waziri wa Nishati, Dk. Doto Mashaka Biteko wakati wa hafla ya kuwasha umeme katika kijiji cha Ikwavila, wilayani Wanging’ombe, Mkoa wa Njombe, Februari 21, 2024.

Viongozi wengine walioshiriki katika hafla hiyo ya kuwasha umeme ni pamoja na Mkuu wa Mkoa wa Njombe, Anthony Mtaka, Mkuu wa Wilaya ya Wanging’ombe Claudia Kitta na viongozi wengine wa Vyama vya Siasa na Serikali.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
591,000SubscribersSubscribe

Latest Articles