Na Patricia Kimelemeta, Dar es Salaam
MKURUGENZI wa Kituo Cha Sheria na Haki za Binadamu(LHRC), Dk. Hellen Kijo-Bisimba amenusurika kifo ajalini.
Dk. Kijo-Bisimba alipata ajali mbaya ya gari katika daraja la Salender Dar es Salaam jana.
Katika ajali hiyo, Dk. Kijo-Bisimba anadaiwa kuvunjika mguu mmoja baada ya gari lake kupoteza mwelekeo na kupinduka mara nne.
Ajali hiyo ilitokea jana asubuhi wakati akitoka kusali eneo la Posta akitumia gari dogo ya Toyota Prado namba T 159 ATY.
Mkurugenzi wa Fedha na Utawala wa LHRC, Ezekiel Masanja alisema baada ya kupata taarifa ya ajali hiyo alikwenda na kumchukua Dk. Kijo-Bisimba.
Alisema alimpeleka katika Hospitali ya Agha Khan kwa matibabu.
Masanja alisema vipimo vya awali vilionyesha amevunjika mguu lakini hadi jana jioni madaktari walikuwa wakiendelea kumuangalia zaidi.
Kamanda wa Polisi Mkoa wa Kinondoni, Camillus Wambura alikiri kutokea tukio hilo akisema polisi wanaendelea na uchunguzi wa ajali hiyo.
“Sina maelezo yanayojitokeza kuhusu ajali hii kwa sababu askari wanaendelea kufanya uchunguzi kujua chanzo chake,”alisema Wambura.
Mashuhuda walisema gari la Dk. Kijo-Bisimba liligongwa ubavuni na gari nyingine iliyokua inatoka la Sea View kwenda barabara ya Ali Hassan Mwinyi.
Walisema gari hilo lilikua linaendeshwa na kijana ambaye hakufahamika na baada ya kuligonga gari la Kijo-Bisimba lilizunguka mara nne na kupinduka.
Katika gari la Dk. Kijo-Bisimba walikuwamo watu wawili na inadaiwa gari lililomgonga lilikuwa likiendeshwa na kijana wa miaka 13.