Safina Sarwatt-KILIMANJARO
KATIBU Mkuu wa Chama cha Mapinduzi (CCM), Dk. Bashiru Ally, amesema Mbunge wa Vunjo, James Mbatia (NCCR-Mageuzi) na mwenzake wa Hai, Freeman Mbowe (Chadema), wamekuwa wakifanyakazi ya utekelezaji wa ilani ya uchaguzi ya CCM.
Mbali na Mbatia, pia aliwataja wabunge Zitto Kabwe wa Kigoma Mjini (ACT Wazalendo) na Mchungaji Peter Msigwa wa Iringa Mjini (Chadema).
Hayo aliliyasema jana mjini Moshi, alipokuwa akizungumza na mabalozi wa mashina ambapo alisema wabunge hao wamekuwa wakifanyakazi ya chama tawala CCM kwa sababu hawana serikali wala Ikulu na kwa sasa wanafanyakazi kwa maelekezo ya CCM.
Pamoja na hali hiyo, alitoa onyo kwa Zitto ambaye pia ni Kiongozi wa Chama cha ACT Wazalendo na kusema si wa viwango vyake huku akimtaka kumtomzoea.
“Mbatia ni mtu mwelewa sana sisi kama chama tutakaa nae tumpe malekezo na kwamba hatuna wasiwasi nae kabisa. Msingwa pia na Zitto hawana shida wale ni watu wetu wanaisaidia CCM kutekeleza ilani ya uchaguzi ya chama .
“Mbowe tutampa malekezo,tunajua na jana nilikuwa jimboni kwake Hai , nilipokelewa vizuri na watu wake wameniahidi wako tayari,” alisema Dk. Bashiru
Aliwataka wananchi waendelee kuchapa kazi ili kujenga uchumi wa nchi na katu waepuke kuishi maisha ya anasa.
Alisema majimbo saba ya Mkoa wa Kilimanjaro yote yamekuwa ya CCM, hata wapinzani wanalitambua hilo.
Alisema majimbo ya Moshi Mjini ,Vunjo, Moshi Vijijini, Same Mashariki na Rombo hayo ni majimbo yaongozwa na upinzani, yatarudi CCM kwa sababu wakuu wa wilaya ni wa chama hicho na Serikali.
Alisema chama hicho hakijaahidi kuwagawia wananchi fedha zaidi ya maendeleo kwa wananchi.
Katibu wa CCM Mkoa wa Kilimanjaro, Jonathan Mabihya alisema uchaguzi ujao, chama hicho kitashinda majimbo yote.