Mwandishi Wetu, Dar es Salaam
Katibu Mkuu wa Chama Cha Mapinduzi (CCM), Dk. Bashiru Ally, ameitaka Marekani na taasisi za kimataifa kuheshimu uhuru wa Tanzania.
Amesema kauli iliyotolewa na Marekani kuhusu uchaguzi mdogo wa marudio uliofanyika Agosti 12, mwaka huu katika maeneo mbalimbali nchini, inagusa maeneo mengi na ni matarajio yake kwamba taasisi zote za nchi zinazohusika zitazingatia madukuduku yao.
Kauli hiyo ya Dk. Bashiru imekuja siku mbili baada ya Ubalozi wa Marekani kutoa tamko kuhusiana na uchaguzi huo ambapo ilisema uligubikwa na vurugu na pia haukufuata sheria.
“Nimeisoma na nimeielewa, sisi kama chama, tunazingatia zaidi uhuru wa kitaifa kwamba taifa hili ni taifa huru na CCM kina dhamana ya kusimamia uhuru wa kitaifa.
“Ninachojua mimi chaguzi zote zimefanywa kwa msingi wa sheria na matarajio yangu ni kwamba Marekani na taasisi nyingine za kimataifa, zitaheshimu uhuru wa taifa letu,” amesema Dk. Bashiru akihojiwa Kituo cha Deustche Welle cha Ujerumani.