MKALI wa mchezo wa tenisi, Novak Djokovic, amefanikiwa kumbwaga mpinzani wake, Andy Murray, katika fainali za michuano ya wazi ya Australia na kutwaa ubingwa jana nchini Australia.
Djokovic alifanikiwa kutwaa ubingwa baada ya kumchapa mpinzani wake kwa seti 6-1, 7-5, 7-6 katika mchezo ambao ulitumia saa mbili na dakika 53.
Nyota huyo alionesha dalili za ubingwa mapema katika seti ya kwanza baada ya kumchapa mpinzani wake 6-1, ambapo mashabiki wa Murray walianza kukata tamaa na ubingwa huo.
Hata hivyo, seti ya pili alijaribu kuonesha makeke yake lakini bado mpinzani wake alizidi kuonesha uwezo wake na kushinda kwa seti 7-5, wakati seti ya mwisho, Djokovic alitawazwa kuwa bingwa baada ya kumaliza kwa seti 7-6.
Ubingwa huo unamfanya uwe wa sita katika michuano hiyo ya wazi ya Australia, wakati Murray akipoteza fainali hizo mara sita.
“Ni furaha kubwa kutwaa ubingwa huu, haikuwa kazi rahisi kwa kuwa mpinzani wangu alikuwa na uwezo wa hali ya juu, lakini nashukuru kufanikiwa kutwaa ubingwa,” alisema Djokovic.