24.1 C
Dar es Salaam
Sunday, September 8, 2024

Contact us: [email protected]

Diwani Kimwanga afanya kikao na wazazi hofu utekaji watoto

Na Mwandishi Wetu, Mtanzania Digital

Diwani wa Kata ya Makurumla Halmashauri ya Manispaa ya Ubungo mkoani Dar es Salaam, Bakari Kimwanga, amewataka wazazi na walezi kuhakikisha wanakuwa na utulivu hasa kutokana na taharuki ya utekaji watoto kwenye shule.

Pamoja na hali hiyo amesema kuwa mpaka sasa ndani ya Kata ya Makurumla hakuna tukio la kutekwa kwa mtoto huku akiweka wazi ni lazima kila mwana jamii ahakikishe anatoa ulinzi kwa mtoto hasa wanapokuwa mitaani.

Kauli hiyo ametoa Julai 23, 2024 alipokuwa akizungumza na wazazi, walezi na walimu katika shule za Msingi za Mianzini, Karume na Dk. Omari, ambapo juzi ilizuka taharuki ya kutekwa watoto kwenye shule hizo na kuibua Sintofamu kwa wazazi kulazimika kuvamia shule ili kuona usalama wa watoto wao.

“Tangu zilipoibuka taarifa hizi za taharuki Julai 22, 2024 (Jumatatu), tumefuatilia taarifa kwenye shule zetu, vyombo vya ulinzi na usalama kwa maana ya Jeshi la Polisi hali iko shwari wazazi wenzangu.

“Wale waliopata taharuki na kuja shule hawajakosea kwa sababu wamefanya hivyo kwa lengo la kutaka kujua usalama wa watoto. Najua mama zetu uchungu mkubwa wanaoupata hasa kuhusu watoto. Wazazi wenzangu naomba tuwe na tulivu hali iko shwari kubwa tusisahau wajibu wetu wa malezi na usalama kwa watoto hata wanapokuwa nyumbani,” amesema Diwani Kimwanga

Aidha, amewataka wazazi kutambua kuwa ni lazima wanaweka mkazo kwenye suala la lishe kwa watoto kwa kuhakikisha wanachangia Shilingi 500 ya chakula kama walivyokubaliana kwenye mikutano ya wazazi jambo ambalo litamsaidia mtoto kupata chakula shuleni badala ya kwenda mitaani wakati wa kipindi cha mapumziko

Kwa upande wake Afisa Elimu Msingi, Manispaa ya Ubungo, Denis Nyoni amewataka wazazi kuwa na utulivu kwani hadi kufikia jana hakuna taarifa za watoto kutekwa katika shule kwenye manispaa hiyo.

“Naomba walimu msisahau wajibu wa kuandika mahudhurio ya watoto kila siku wawapo darasani na hata wakati wanapomaliza masomo kwa siku majina yaitwe. Hatua hii ndio njia ya kuendelea kudhibiti usalama wa watoto wetu,” amesema Nyoni

Naye Polisi Kata ya Makurumla, Insp Emmanuel Humba, amesema kuwa katika Kata ya Makurumla hali ni shwari hakuna tukio la utekaji kwa watoto huku akiwaomba wazazi wawe na utulivu wanapopata taarifa za taharuki.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
589,000SubscribersSubscribe

Latest Articles