Na RENATHA KIPAKA-KARAGWE
KATIBU wa Hospitali Teule ya Nyakahanga iliyopo wilayani Karagwe mkoani Kagera, Jeremia Lugimbana, amesema hali ya Diwani wa Kata ya Nyakahanga, Charles Bechumila (CCM), aliyejeruhiwa vibaya kwa kushambuliwa kwa mishale inaendelea vizuri.
Akizungumza na gazeti hili juzi, Lugimbana, alisema diwani huyo alifikishwa hospitalini hapo akiwa na hali mbaya na kupelekwa kwenye chumba cha upasuaji kwa ajili ya kumshona sehemu alizojeruhiwa na sasa hali yake inaendelea vizuri.
“Ni siku ya nne tangu diwani huyo ameletwa hapa akiwa hajitambui pamoja na majeraha tulimpokea na kumwingiza katika chumba cha upasuaji kwa ajili ya kuanza kuzishona sehemu zilizokuwa na majeraha makubwa na kwa sasa bado anaendelea na matibabu na hali yake inaendelea vizuri,” alisema.
Diwani huyo alijeruhiwa vibaya kwa kushambuliwa kwa mishale baada ya msafara wa Mkuu wa Wilaya ya Karagwe mkoani Kagera, Godfrey Mheluka, kushambuliwa na wananchi katika Kijiji cha Kashanda, Kata ya Nyakahanga wakati wakiwa wamekwenda kufuatilia mgogoro wa wafugaji na wakulima.
Ilidaiwa kuwa Mheluka alikwenda kijijini hapo kwa ajili ya kutoa tamko kuhusiana na mgogoro wa wakulima na wafugaji akiwa na msafara wa magari mawili na katika gari lake alikuwa ameambatana na Katibu Tawala wa Wilaya (DAS), Innocent Msena, ofisa uhamiaji mmoja na askari polisi wawili.
Gari la pili katika msafara huo lilikuwa na Bechumila, maofisa tarafa wawili na waandishi wa habari wawili wa Redio Karagwe.
Kwa mujibu wa mashuhuda wa tukio hilo, baada ya kufika kijijini hapo, Mheluka na msafara wake waliacha magari umbali wa mita 600 na kwenda kuangalia eneo lililokuwa likidaiwa kuwa na mgogoro baina ya wakulima na wafugaji, lakini wakiwa njiani walikuta wakulima wawili wakiwa wanaendelea na shughuli zao za kilimo na kuagiza wakamatwe.
“Baada ya kuwakamata wakulima hao, walinyoosha mikono juu, nadhani walitoa ishara kwa wenzao, kitendo hicho kilisababisha kuanza kushambuliwa kwa mishale, ilianza kurushwa na makundi ya watu kutoka maeneo mbalimbali hali iliyowalazimu polisi waliokuwa kwenye msafara huo kuanza kujibu kwa kufyatua risasi huku DC na msafara wakikimbilia kwenye magari,” alieleza mmoja wa shuhuda hao.
Alisema hali ilizidi kuwa mbaya kutokana na mashambulizi ya wanakijiji kuendelea lakini wakati wakiwa katika harakati za kujiokoa kwa kukimbilia kwenye magari, diwani alipigwa mishale na kuanguka chini hivyo kuwafanya polisi kuzidisha mashambulizi ya risasi kuwaokoa na kufanikiwa kuwatawanya wakulima na kumwokoa diwani.
Kamanda wa Polisi Mkoa wa Kagera, Augostino Ulomi, alisema wameanza hatua za kuwatafuta watu waliohusika na tukio hilo na tayari 15 wamekamatwa na kufikishwa katika kituo cha polisi.