Mwandishi Wetu na Mashirika ya Habari
MFANYABIASHARA Mohammed Dewji pamoja na Mbunge wa zamani wa Igunga, Rostam Aziz, ndio matajiri zaidi Tanzania.
Kwa mujibu wa orodha mpya ya mabilionea ya mwaka 2015 iliyotolewa na mtandao wa Forbes, Dewji ameshika nafasi ya kwanza nchini akiwa mbele ya Rostam.
Awali nafasi ya kwanza kwa Tanzania ilikuwa ikishikiliwa na mfanyabiashara Rostam.
Dewji (39), mfanyabiashara ambaye pia ni mbunge wa Singida Mjini kupitia CCM, anatajwa na Forbes kuwa na utajiri wa dola za Marekani bilioni 1.3 unaomfanya ashike nafasi ya 1,500 duniani na 31 barani Afrika.
Kwa upande wake, Rostam aliyetajwa kuwa na utajiri wa dola za Marekani bilioni moja, anashika nafasi ya 1,741 duniani, 32 barani Afrika na wa pili nchini.
Kwa mujibu wa Forbes, licha ya kushuka kwa bei ya mafuta na kudhoofu kwa sarafu ya Euro, hadhi ya kifedha ya matajiri wa dunia katikati ya matatizo ya kiuchumi imepanda kwa mara nyingine.
Katika orodha hiyo ya 29 ya matajiri, Forbes ilisema mwaka huu ulivunja rekodi kwa kuingiza mabilionea 1,826 wenye utajiri wenye thamani ya dola trilioni 7.05 kutoka trilioni 6.4 mwaka jana.
Bill Gates ameendelea kuwa mtu tajiri duniani taji alilolishika mara 16 katika kipindi cha miaka 21 iliyopita. Utajiri wake ulikua kwa dola za Marekani bilioni 3.2 tangu mwaka jana na kufikia dola bilioni 79.2.
Hata hivyo, tajiri kuliko wote barani Afrika, Aliko Dangote wa Nigeria, licha ya kutetea hadhi yake, utajiri wake umeshuka hadi dola za Marekani bilioni 14.7 kutoka dola bilioni 25 mwaka jana kutokana na udhaifu wa sarafu ya Nigeria.