MWANDISHI WETU
KWA muda mrefu, utamaduni wa kubeba watoto mgongoni umekuwa sehemu ya malezi katika jamii nyingi za Kiafrika. Tangu mtoto anapozaliwa, wanafamilia hupokezana kumshika na kumbeba kama namna ya kuonesha furaha yao. Ni nadra mtoto mchanga kubaki mwenyewe kitandani isipokuwa katika nyakati fulani fulani.
Sambamba na kubebwa mgongoni, mtoto huyu hulala kitanda kimoja na wazazi wake hadi hapo atakapofikia umri wa kuhamia chumba kingine aweze kulala na wenzake.
Jamii nyingine nje ya Bara la Afrika zinapata shida kuelewa desturi hii. Kwao ni rahisi kufikiri kuwa kumweka mtoto mgongoni ni aina fulani ya ukatili na kumkosea mtoto haki ya kuwa huru. Katika jamii hizo, watoto huzoezwa maisha ya upekee tangu wanapokuwa wadogo.
Pamoja na tofauti hiyo ya kiutamaduni, mambo yameanza kubadilika kwa kasi hapa kwetu. Imeanza kuwa kawaida kwa wazazi kuwaandalia watoto vitanda vyao tangu wanapozaliwa. Watoto wameanza kulala peke yao. Ule utaratibu wa kubebwa kifuani au mgongoni mwa mzazi wake pia umeanza kupotea. Badala yake, wazazi huwaweka watoto katika vifaa maalumu wanapokuwa matembezini sambamba na kuwalaza kwenye vitanda vya kujitegemea.
Zipo sababu nyingi zinazoweza kueleza kwanini mambo yamebadilika. Kwa mfano, kuna suala la mwingiliano wa utamaduni baina ya jamii mbalimbali. Hivi sasa, mathalani, ni rahisi kwa mzazi wa Simiyu kujua mtindo wa maisha ya wazazi wa barani Ulaya na hivyo kubadili kabisa namna anavyoishi.
Lakini pia, mwingiliano huu unapokwenda sambamba na kuimarika kwa uwezo wa kiuchumi, inakuwa rahisi kwa wazazi kubadili namna yao ya maisha. Wazazi wenye kipato cha kati, wanaweza kutengeneza kitanda maalumu kwa ajili ya mtoto mchanga kwa sababu wanao uwezo huo.
Pamoja na mabadiliko haya, ni muhimu kuelewa kuwa utamaduni huu wa kubeba watoto ni suala la kimaumbile kuliko lilivyo kiutamaduni.
Kisayansi, watoto huzaliwa na hitaji ndani yao la kuunganishwa kimahusiano na watu wengine. Wanazaliwa na njaa ya kutengeneza ukaribu na watu.
Tujenge mazoea ya kuwakumbatia mtoto kila inapowezekana. Kuwakumbatia kunawahakikishia kuwa wako salama.