MSHAMBULIAJI wa timu ya Manchester United, Memphis Depay, ameweka wazi kwamba kufukuzwa kwa kocha wa klabu hiyo, Van Gaal kutampa nafasi mchezaji huyo ya kufanya vizuri.
Mshambuliaji huyo wa pembeni wa timu ya Taifa ya Uholanzi, amesema alishangazwa na kocha huyo kumweka benchi katika fainali ya Kombe la FA dhidi ya Crystal Palace huku United ikichukua ubingwa.
Mchezaji huyo amefanikiwa kufunga mabao mawili katika Ligi Kuu baada ya kucheza michezo 29 tangu asajiliwe kwa kitita cha pauni milioni 25 akitokea PSV Eindhoven msimu uliopita.
“Sijui kama kulikuwa na tatizo kati yangu na Van Gaal, lakini kwa sasa ameondoka na ndivyo ilivyo katika maisha ya soka, unatakiwa kujifunza ili kuja kuwa bora.
“Ninaamini ujio wa Mourinho katika klabu hii hali yangu itakuwa shwari na nitafanya makubwa kama atanipa nafasi na nitamuuliza Wesley Sneijder anieleze tabia ya Mourinho ikoje ili niweze kwenda naye sawa,” alisema Depay.