Ramadhan Hassan -Chemba
MKUU wa Wilaya ya Kilolo mkoani Iringa, Asia Abdallah, amesema hatua kali zitachukuliwa kwa wazazi watakaokiuka agizo la kutowapeleka watoto wao shule katika wilaya za Chemba na Kondoa.
Akizungumza juzi katika Kijiji cha Magadi, Kata ya Soya Wilaya ya Chemba mkoani Dodoma wakati wa sherehe za Maulid, Asia alisema hakuna kisingizio cha kutokumpeleka mtoto shule kwani Serikali imeondoa vikwazo vyote ikiwemo ada na michango mingine mashuleni.
“Rais anapeleka mabilioni ya fedha kila mwezi, zaidi ya Sh bilioni 23 kwa ajili ya watoto wetu wapate elimu bila malipo, zamani sisi tulikuwa tunasoma tunajilipia ada, sasa hivi hakuna,” alisema Asia.
Vilevile aliwataka viongozi wa dini wa wilaya hizo kuwahamasisha waumini na wananchi kujitokeza kwa wingi kumpigia kura Rais John Magufuli katika Uchaguzi Mkuu wa Oktoba ili kuleta maendeleo chanya kwa taifa.
Alisema katika historia, wilaya za Chemba na Kondoa kuna changamoto ya watu kutokujitokeza kupiga kura hivyo ni jukumu lao sasa kupambana kumpigia kura Rais Magufuli.
“Kila mwananchi akitambua wajibu wake tutafika mbali sana, Rais wetu anafanya kazi ngumu sana na kama mnafuatilia habari mbalimbali kwenye Tv, redio na mitandao ya kijamii utaona nchi hii ilikuwa masikini na ilipanga kufikia uchumi wa kati 2025 na kabla haujafika tayari tumeingia kwenye uchumi wa kati, ni dhahiri nchi hii siyo masikini, tunahitaji viongozi wa aina ya kina Magufuli, na wananchi tushirikiane kwa pamoja ili tuondokane na wimbi hii la umasikini,” alisema Asia.
Alitoa rai kwa mashekhe na jamii kwa ujumla kufanya kazi kwa bidii na kuachana na mambo yasiyokuwa na tija ili kuleta heshima kwa taifa.
Asia alisema alikuwa na mpango wa kutia nia kugombea ubunge wa Viti maalumu Mkoa wa Dodoma, lakini ameshindwa kutokana na kutii mamlaka ya rais kwakuwa bado anahitaji kuendelea kumsaidia katika majukumu yake ya kufanya kazi katika Wilaya ya Kilolo.
“Katika vitabu vya dini mnatambua tumeelekezwa kutii mamlaka, hivyo nimetii mamlaka ya uteuzi wangu, mimi ni nani mpaka niwe na kiburi mbele ya kiongozi wangu nisitii mamlaka,’’ alisema Asia.
Naye, mwalimu wa madrasa, Aisha Mohamed aliwataka wazazi kuwalea watoto wao katika maadili mema ili kuwa na kizazi chenye utii siku za mbeleni.