25.3 C
Dar es Salaam
Monday, July 4, 2022

Kampuni yaja na teknolojia ya lami baridi kujenga barabara

Ramadhani Hassan -Dodoma

KAMPUNI ya Starpeco Limited ya Dar es Salaam, imeanza ujenzi wa barabara darasa jijini hapa kwa kutumia teknolojia ya lami baridi huku Wakala wa Huduma za Barabara Vijijini (Tarura) ikisema iwapo teknolojia hiyo itaonekana kufanya  vizuri  watairuhusu iweze kutumika maeneo mbalimbali nchini.

Hayo yalielezwa jana jijini hapa na Meneja wa Tarura Mkoa wa Dodoma, Mhandisi Mohammed Makwata  wakati akifungua semina ya wanafunzi  wa vyuo vya ufundi stadi (Veta) nchini ambao walikuwa wakipewa uelewa kuhusu teknolojia ya lami baridi.

Semina hiyo iliandaliwa na Kampuni ya Starpeco ambayo inajishughulisha na ujenzi wa barabara kwa kutumia lami baridi.

Makwata alisema iwapo  teknolojia ya lami baridi itaonekana kufanya  vizuri,  watairuhusu iweze kutumika maeneo mbalimbali nchini kwani wana mtandao mkubwa wa barabara.

“Teknolojia hii ikionekana kufanya vyema basi itatumika katika ujenzi wa barabara zetu. Tarura ina barabara nyingi zinazohitaji kujengwa na kutumika nyakati zote kwa maendeleo ya uchumi wa nchi,” alisema Makwata.

Kwa upande wake, Mkurugenzi wa Starpeco, Gratian Nshekanabo, alisema kampuni yake  imeweza kuweka  viraka katika barabara ya Changanyikeni na barabara ya Uvumbuzi zilizopo Chuo Kikuu cha Dar es Salaam, pamoja na kumwaga lami mpya katika barabara ya Kileleni yenye urefu wa kilomita 120.

Pia alisema teknolojia ya lami baridi imetumika katika ujenzi wa barabara ya Bagamoyo, Tazara Flayover na Ubungo Flyover na kwa sasa wanakarabati barabara darasa katika Jiji la Dodoma.

Alizitaja barabara hizo ni zile zenye majina ya viongozi wakuu wa nchi ambazo ni Magufuli na Samia zilizopo Area C jijini hapa.

Nshekanabo alisema teknolojia hiyo ni nzuri kwa kuwa ni rafiki kwa mazingira, ni rahisi na gharama zake ni ndogo, hivyo aliitaka Serikali kuitumia katika ujenzi wa barabara zake.

“Ujenzi wa lami  baridi kuna faida nyingi na ni rafiki kwa mazingira, ni rahisi. Tuache mazoea kwani  mambo yamebadilika, tunaweza tukawa tunawalalamikia wakandarasi wakati hawatakiwi kulalamikiwa,  tubadilike tutumie lami baridi,” alisema Nshekanabo. 

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
195,649FollowersFollow
545,000SubscribersSubscribe

Latest Articles