Renatha Kipaka, Muleba
Mkuu wa Wilaya ya Muleba, Toba Nguvila amewasihi Madiwani kuendelea kusimamia kikamilifu miradi yote inayotekelezwa na Serikali ndani ya Halmashauri hiyo.
Nguvila emetoa wito huo leo Ijumaa Februari 11, 2022 wakati wa Kikao cha Baraza la Madiwani cha Robo ya Pili ya Mwaka kilichofanyika wilayani Muleba.
Nguvila amewataka madiwani kuhakikisha miradi yote ya Halmashauri na taasisi zingine za serikali ikiwamo ya TARURA, RUWASA, TANESCO na TANROAD kuhakikisha wanaisimamia kwa sababu inawagusa wananchi ambao ndio wapiga kura wao.
“Niwaombe sana miradi yote inayotekelezwa ndani ya kata zenu simamieni, kila wakati tengeni muda kupita kukagua na kama kuna shida waiteni wataalamu waje kufanya ufafanuzi kama kukiwa na shida au kasoro yoyote katika mradi wowote ule iteni wataalamu wanaohusika na mradi huo wafike kutatua kasoro hizo kabla ya mradi haujamalizika,” ameeleza Nguvila.
Aidha, amekemea kitendo cha utoroshaji wa mapato kwa kuwaeleza kuwa pasipo kusimamia mapato Halmashauri haitaweza kutimiza majukumu yake ikiwemo miradi ya maendeleo.
Aidha, amewasihi madiwani kuhakikisha wanasimamia ipasavyo katika kata zao ili kuondoa uvuvi haramu kwa kuwaeleza kuwa uvuvi haramu ukiendelea unadhoofisha mapato ya Halmashauri na ajira zitapotea na samaki watapungua na kutoweka.
Naye Mwenyekiti wa Halmashauri hiyo,Magongo Justus amesema kuwa amemuagiza Mwenyekiti wa Kamati ya Maadili kuanza kushughulikia suala la uvujishaji wa nyaraka ya Halmashauri ili kama ni Madiwani hatua za kimadili ziweze kuchukuliwa dhidi yao.
Katika Mkutano huo, Mhandisi wa Ujenzi, Charles Solo kwa niaba ya Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri amewasilisha taarifa ya mpango wa serikali juu ya zoezi la Anwani za makazi kwa kueleza kuwa ni mfumo wa miundombinu inayokwenda kurahisisha utambulisho wa mahali ambapo mtu anaishi, alipo, biashara yake au ofisi anayofanyia kazi kwa kufuata jina la barabara na mtaa, namba ya nyumba au jengo na Postikodi.