NA VICTOR BARIETY, GEITA TAASISI ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (Takukuru), imewapandisha kizimbazi katika Mahakama ya Wilaya ya Chato, Mkuu wa Wilaya ya Uvinza, Hadija Nyembo na aliyekuwa Mkurugenzi wa Wilaya ya Chato, Hamida Kwikega, kwa tuhuma za upotevu wa Sh bilioni 1.4 za pembejeo za kilimo zilizotolewa na Serikali kupitia Wizara ya Kilimo, Chakula na Ushirika. Mbali na viongozi hao, wengine waliofikishwa mahakamani hapo jana ni Ofisa Kilimo na Mifugo wa Wilaya ya Chato, Phares Tongola na aliyekuwa mwanasheria wa halmashauri hiyo kabla ya kuhamishiwa Manispaa ya Musoma, Robert Matungwa. Wengine ni maofisa kilimo Gordwin Kazahula, Elihuruma Delingo na aliyekuwa wakala wa usambazaji pembejeo katika Kijiji cha Bupandwampuli wilayani Chato. Washtakiwa hao walisomewa mashtaka yanayowakabili mbele ya Hakimu Jovith Katto ambapo Mwendesha Mashtaka wa Takukuru, Osborn Paissi alidai kwa nyakati tofauti kati ya mwaka 2010 na 2011 watuhumiwa hao walitenda makosa huku wakijua kufanya hivyo ni kinyume na sheria. Alisema aliyekuwa mkuu wa wilaya hiyo, mkurugenzi wa halmashauri, mwanasheria, ofisa kilimo na mifugo na maofisa wengine wa Idara ya Kilimo, wanashtakiwa kwa makosa matatu ambapo kila mmoja alitumiwa kutumia madaraka yake vibaya kinyume na sheria. Katika makosa mengine, mwendesha mashtaka huyo wa Takukuru, alidai viongozi hao pamoja na wakuu wa idara wameisababishia hasara Serikali ya Sh bilioni 1.4 pamoja na kusaidia kutenda kosa. Mwendesha Mashtaka Paissi, alisema kwa upande wa aliyekuwa msambazaji wa pembejeo za kilimo, yeye anakabiliwa na makosa 152 yakiwamo ya kutumia nyaraka kwa lengo la kumdanganya mwajiri pamoja na kughushi vocha za pembejeo zilizotakiwa kwenda kwa wakulima. Baada ya kusomewa mashtaka hayo, watuhumiwa hao wote walikana kuhusika na makosa hayo, ambapo Hakimu Katto aliahirisha shauri hilo hadi Machi 27, mwaka huu litakapokuja mahakamani hapo kwa ajili ya kutajwa tena. Hata hivyo, watuhumiwa wote wako nje kwa dhamana baada ya kutimiza masharti kama walivyotakiwa na mahakama. Fedha hizo za pembejeo za kilimo zilitolewa katika msimu wa kilimo wa mwaka 2010 katika Halmashauri ya Wilaya ya Chato na kusimamiwa na viongozi wa wilaya hiyo akiwamo aliyekuwa Mkuu wa Wilaya, Nyembo kabla ya kuhamishiwa Wilaya ya Uvinza mkoani Kigoma.