Na Samwel Mwanga, Maswa
MKUU wa Wilaya ya Maswa mkoani Simiyu, Aswege Kaminyoge amekagua maendeleo ya ujenzi wa Miradi ya Mfuko wa Maendeleo ya Jamii (TASAF) wilayani humo inayotokana na fedha za OPEC na kutaka kasi iongezwe ili iweze kukamilika na itumike kwa manufaa ya wananchi.
Miradi iliyokaguliwa ni Ujenzi wa Bweni la Wasichana katika shule ya sekondari Budekwa ambao uko katika hatua ya jamvi na Ujenzi wa nyumba ya Mganga katika Zahanati ya kijiji cha Mwabayanda(M) ambayo imefikia hatua ya ufungaji Renta.
Miradi mingine ni pamoja na Ujenzi wa Vyumba viwili vya madarasa, ofisi moja ya Walimu na Matundu sita ya Vyoo katika shule ya msingi Mwabujiku ambao umefikia hatua ya kunyanyua kuta na Ujenzi wa nyumba moja ya Walimu watakaoishi wawili ambao umefikia hatua ya kunyanyua ukuta.
“Mratibu wa Tasaf ongezeni kasi ya usimamizi wa miradi hii kwani fedha zote za miradi hii zimeshaletwa na Rais Samia Suluhu Hassan pia mna gari mpya na mafuta ya gari kwa ajili ya ufuatiliaji wa miradi hii mnayo hivyo itembeleeni mara kwa mara na kama kuna changamoto za kutukwamisha fikeni ofisi ya Mkuu wa Wilaya mnieleze.
“Watendaji wa vijiji na kamati zilizoundwa kwa ajili ya kusimamia miradi hii hakikisheni kasi inaongezeka ya ujenzi ili miradi hii iweze kutumika kama ilivyokusudiwa na serikali,” amesema Kaminyoge.
Ameagiza vifaa vyote vya ujenzi katika miradi ya vijiji vya Budekwa, Mwabujiku na Igunya vipelekwe mara moja ili kazi ziendelee kwa kuwa hataki kuona miradi iliyoletwa na serikali katika wilaya hiyo inasuasua katika kukamilika.
Aidha, amewataka viongozi wa Kata na Vijiji ambapo miradi hiyo inatekelezwa wahakikishe wanawahamasisha na kuwasimamia wananchi kuhakikisha wanatumia nguvu zao katika kukusanya mchanga, mawe, kokoto na kuchoto maji.
“Katika miradi hii inayotekelezwa na Tasaf ni miradi ya serikali hivyo Maafisa Watendaji wa Kata na Vijiji ambapo miradi hii inajengwa hamasisheni wananchi watumie nguvu zao kuleta mchanga, kokoto,mawe na maji maana hakuna mwananchi hata mmoja kuchangishwa fedha,” amesisitiza.
Nae Mratibu wa Tasaf wilaya ya Maswa, Grace Tungaraza amemhahidi mbele ya Mkuu huyo wa wilaya kutekeleza maagizo yote aliyoyatoa na kuzipatia ufumbuzi changamoto ambazo zimejitokeza wakati wa ujenzi wa miradi hiyo inaendelea hasa ile ambayo kasi yake bado ni ndogo.
“Maagizo yote yaliyotolewa na Mkuu wa wilaya baada ya kupitia miradi hii ambayo tunaisimamia sisi tutayatekeleza na hizi changamoto zilizojitokeza tutahakikisha tunazimaliza ili hii miradi ikamilike na tuweze kuletewa fedha nyingine,” amesema.