Na Nora Damian, Mtanzania Digital
Mkuu wa Wilaya ya Ilala, Ng’wilabuzu Ludigija, amewataka wananchi kufanya usafi kuwa endelevu kwa kuwa wamejipanga kuhakikisha wilaya hiyo inakuwa safi wakati wote.
Akizungumza wakati wa usafi wa pamoja uliofanyika katika Mtaa wa Kongo na Agrey Kata ya Kariakoo, amesema kila Jumamosi ya mwisho wa mwezi wamekuwa wakichagua sehemu moja ambapo yeye kwa kushirikiana na wakuu wa idara, kampuni za usafi na wananchi wanashiriki kufanya usafi.
“Zoezi la safisha pendezesha Dar es Salaam ni endelevu na tutahakikisha tunalisimamia kwa nguvu zetu zote, hatutaki tusubiri mpaka inyeshe mvua halafu kutokee mlipuko wa magonjwa tuanze kuhangaika kutumia rasilimali za taifa kutibu watu wakati tungeweza kuchukua hatua na kuzuia,” amesema Ludigija.
Mkuu huyo wa wilaya pia amewataka wafanyabiashara waliokuwa wamepanga meza katika makutano ya Mtaa wa Kongo na Uhuru kuziondoa ili barabara ziweze kupitika wakati wote.
“Tunataka maeneo yote ya Kariakoo yapitike wafanyabiashara msisubiri mpaka viongozi tunakuja kufanya usafi kwenye maeneo yenu, tutakuwa tunapita tukikuta takataka na watu wanafanya biashara tutachukua hatua kwa mujibu wa sheria,” amesema.
Pia amewaagiza maofisa mazingira, maofisa afya na watendaji wa mitaa na kata kupita kwenye majengo kubaini waliounganisha mabomba yao katika mitaro ya maji ya mvua.
Naye Mkuu wa Idara ya Mazingira na Udhibiti Taka Ngumu wa Halmashauri ya Jiji la Dar es Salaam, Rajabu Ngoda, amesema watatekeleza maagizo yote yaliyotolewa na mkuu wa wilaya na kuwataka wananchi na wafanyabiashara kushiriki kikamilifu kuliweka jiji safi.
Kwa upande wake Kiongozi wa Wamachinga, Yusuf Namoto, amesema wataunda kamati maalumu ya usimamizi wa mazingira ili kuhakikisha kila mfanyabiashara kabla ya kufungua na kufunga biashara yake anafanya usafi wa eneo lake.