Na Waandishi wetu – Dar es Salaam
BAADA ya Jeshi la Polisi kumshikilia kwa zaidi ya saa 48 Mbunge wa Kawe, Halima Mdee, Mkuu wa Wilaya ya Kinondoni, Ally Hapi, ambaye ndiye chanzo cha kukamatwa kwa mwanasiasa huyo, amejivua kwenye sakata hilo.
Jana jeshi hilo lilimuhamisha Mdee kutoka katika mahabusu za Kituo cha Oysterbay alikokaa kwa siku nne na kumpeleka Kituo Kikuu cha Polisi (Central), ambako anaendelea kushikiliwa kwa kosa la uchochezi.
MTANZANIA Jumapili lilipomtafuta Hapi ili kufahamu kama amri ya saa 48 alizozitoa kwa polisi kumshikilia Mdee ina mabadiliko yoyote, alisema kwa sasa suala hilo asiulizwe yeye bali Jeshi la Polisi.
“Muulizeni Kaimu wa Polisi Kanda Maalumu ya Dar es Salaam,” alisema Hapi bila kufafanua.
MTANZANIA Jumapili lilipomtafuta Kaimu Kamanda wa Polisi Kanda Maalumu ya Dar es Salaam, Lucas Mkondya na kumuuliza kuhusu hilo, alijibu kuwa yuko likizo.
“Niko likizo, sijui kama (Mdee) yupo hapo, mtafute Kamanda wa Polisi Mkoa wa Ilala,” alisema Mkondya.
Alipotafutwa kwa simu Kamanda wa Polisi Mkoa wa Ilala, Salum Hamduni, alikiri kuwa ni kweli mbunge huyo alipelekwa hapo kwa mahojiano.
“Aliletwa hapa kwa mahojiano, lakini ni suala la Kanda Maalumu,” alisema Kamanda Hamduni.
Alipoulizwa msingi wa mahojiano hayo, Kamanda Hamduni alisema kuwa hilo ni suala la kipelelezi kupitia Kanda Maalumu.
“Mimi si mpelelezi, anayepeleleza ni Kanda Maalumu,” alisema.
Mdee ambaye alihojiwa kwa saa kadhaa jana mara tu baada ya kuhamishiwa Kituo Kikuu cha Polisi, hakupatiwa dhamana kwa kile kilichoelezwa askari waliopewa jukumu la kumuhoji hawakuwa na maelekezo mengine.
Awali, MTANZANIA Jumapili lilimtafuta Wakili wa Mdee, Hekima Mwasipu ambaye alifafanua kuwa mteja wake alihojiwa kwa kosa la uchochezi.
“Ni kweli alihamishiwa Kanda Maalumu leo (jana),” alisema Mwasipu.
MTANZANIA Jumapili lilitaka kufahamu sababu za Mdee kuhamishwa kutoka Kituo cha Oysterbay na kupelekwa Kanda Maalumu ambako ameendelea kushikiliwa licha ya saa 48 kupita, Mwasipu alisema hata yeye alihoji na kujibiwa kuwa ni suala la polisi kanda hiyo.
“Sababu za kumtoa kule na kumleta Kanda Maalumu sielewi ni nini, lakini ninachoweza kusema ni kwamba Jeshi la Polisi linafanya kazi kwa kushirikiana.
“Ila kwa maelezo yao hata mimi nilipowahoji walijibu kwamba makosa hayo yako chini ya Kanda Maalumu, ni ‘special’ (maalumu), kesi ziko chini ya kanda hiyo,” alisema Mwasipu.
Alipoulizwa kuhusu hali ya mbunge huyo ambaye awali aligoma kula na suala la dhamana, Mwasipu alisema hivi sasa anakula na alihojiwa kwa takribani saa moja, lakini dhamana yake ilishindikana.
“Suala la kufikiswa mahakamani ama kutofikishwa mahakamani hilo ni suala lao polisi, lakini maelezo kaandika na tulifuatilia suala zima la dhamana ikawa ngumu.
“Walisema wao hawana maelekezo yoyote kuhusu dhamana, ni wale ambao walikuwa wanamsimamia Halima kuandika maelezo, hadi jioni hii walinipigia simu, kimsingi leo hatapata dhamana, labda kesho,” alisema Mwasipu.
Awali, waandishi wa MTANZANIA Jumapili walifika kituoni hapo, lakini walizuiwa getini baada ya kujitambulisha kwa madai kuwa Kaimu Kamanda wa Kanda Maalumu hakuwapo ofisini na wala hakukuwa na mtu mwingine aliyekuwapo ili kutoa taarifa kwa waaandishi wa habari na kutakiwa kusubiri nje ya eneo la kituo.
Wakiwa nje ya kituo hicho ambako walikaa kwa saa kadhaa, walishuhudia hali ya utulivu huku ukaguzi ukiendelea, huku baadhi ya watu waliosadikika kuwa wafuasi wa Chadema walizuiwa kuingia na kukaa kando kwa muda kabla ya kuondoka.
Mdee, ambaye pia ni Mwenyekiti wa Baraza la Wanawake wa Chadema (Bawacha), alikamatwa Julai 4, mwaka huu, baada ya Hapi kutoa amri ya kushikiliwa kwa saa 48 kutokana na matamshi aliyodai kuwa ni ya kumkashifu Rais Dk. John Magufuli.
Matamshi hayo anadaiwa kuyatoa katika mkutano aliofanya na waandishi wa habari Makao Makuu ya Chadema, Kinondoni, Dar es Salaam.
Mdee alidaiwa kumkashifu Rais Magufuli kutokana na kuhoji baadhi ya kauli zake zikiwamo zile alizotumia wakati akitangaza kupiga marufuku wanafunzi wa kike wanaopata mimba kurejea shuleni.
Si hilo tu, Mdee pia alihoji kauli nyingine zinazotolewa na Rais Magufuli ambazo alidai kuwa zinakiuka misingi ya sheria.
ACT –WAZALENDO YALAANI
Wakati huo huo, Chama cha ACT-Wazalendo kimelaani kitendo cha wakuu wa mikoa na wilaya kutumia madaraka yao vibaya kupitia sheria ya Mamlaka ya Serikali za Mitaa, inayowaruhusu kukamata na kumuweka mtu kizuizini kwa saa 48.
Akizungumza Dar es Salaam jana, Katibu Mwenezi wa Ngome ya Vijana wa chama hicho, Karama Kaila, alisema amri ya kuwaweka watu ndani kwa saa 48 inatumiwa vibaya na wateule wa rais na kuigeuza kuwa sehemu ya kuwakomoa watu wenye mawazo tofauti na kauli au matakwa yake.
Alisema vijana wa chama hicho wanaamini katika misingi ya utawala bora kwa viongozi wa umma kuheshimu katiba ya nchi ambayo ni sheria mama wanapokuwa wakitekeleza majukumu yao.
“Katiba inatoa haki kwa kila raia kutoa maoni yake kwa uhuru bila kuvunja sheria za nchi, amri ya Mkuu wa Wilaya ya Kinondoni ni matumizi mabaya ya sheria na uvunjifu wa katiba ya nchi ambayo viongozi wameapa kuisimamia.
“Mdee hajamtukana rais wala hajatoa maneno yoyote yenye viashiria vya uvunjifu wa amani kama alivyodai ndugu Hapi,” alisema Kaila.
CHADEMA YAHOJI
Katika hatua nyingine, Chadema kimehoji Mdee kuendelea kushikiliwa na Jeshi la Polisi kwa takribani saa 72 bila kufikishwa kwenye vyombo vya sheria jambo ambalo kimesema kuwa ni kinyume na sheria za nchi.
Kwa sababu hiyo, Chadema imeendelea kusisitiza msimamo wake wa kukusudia kuchukua hatua za kisheria dhidi ya wakuu wa mikoa na wilaya ambao wamekuwa wakitumia madaraka yao vibaya kupitia Sheria ya Tawala za Mikoa.
Ofisa Habari, Tumaini Makene, alisema tayari chama kimeshawaagiza wanasheria kuanza mchakato kwa hatua za kisheria.