Na RAMADHAN HASSAN
- DODOMA
MKUU wa Wilaya ya Chemba, Simon Odunga ambaye alimcharaza bakora mkazi wa Kijiji cha Kambiyanyasa, Chindika Pingwa (57), amemwomba msamaha mzee huyo pamoja na kutoa mbuzi mmoja kwa ajili ya kupoza mwili wake.
Mkuu huyo wa wilaya amechukua hatua hiyo siku moja baada ya Pingwa kutishia kumpeleka mahakamani kutokana na kitendo hicho cha udhalilishaji.
Mkuu huyo wilaya alifikia hatua hiyo, baada ya mtoto wa Pingwa kuvunja kioo cha gari lake, wakati akicheza na wenzake kando kando ya barabara.
Kutokana na hali hiyo, mkazi huyo alikuja juu na kumtaka mkuu huyo wa wilaya kumwomba radhi akidai amemdhalilisha mbele ya familia yake, vinginevyo anakwenda mahakamani.
Akizungumza na MTANZANIA jana, Pingwa alikiri kuombwa msamaha, kwani juzi mkuu huyo wa wilaya alifika nyumbani kwake na kumwomba radhi kwa kitendo alichokifanya pamoja na kumpatia mbuzi jike kwa ajili ya supu.
Alisema alipewa mbuzi huyo kwa ajili ya supu na kuurudisha mwili wake baada ya kuumizwa sehemu za kichwani, mgongoni na mikononi.
“Alikuja hapa akiwa ameongozana na baadhi ya viongozi alinipa mbuzi jike pia aliniomba radhi kwa yote yaliyotokea. Pamoja na kufika nyumbani juzi lakini jana pia alituomba tufike ofisini kwake na tulifika tukayazungumza kwa kina,”alisema.
Aidha mkuu huyo wa wilaya anagharamia matibabu yake lakini akamtaka pia kuisaidia familia yake kwani yeye ndiye mtafutaji.
“Nimekaa tu nikiuguza haya majeraha kazi sifanyi namwomba aiangalie na familia yangu pia,”alisema.
Alipulizwa kuhusina na kwenda mahakamani,Pingwa alisema: “Siwezi kufanya hivyo kwani amekuja na ametaka tuyamalize na mimi nimekubali yaishe,” alisema.
Kwa upande wake Odunga alipoulizwa alisema amezungumza na mzee huyo na wameyamaliza.
“Huyo Mwananchi tulishakutana nae na alikuwa ofsini kwangu jana(juzi)na nafikiri maswala yake tumeyazungumza kwa kina.
“Nadhani suala lake lilimalizika na yeye alikiri kufanya mambo ambayo sio sahihi lakini kakiri basi kama binadamu yeye alikasirika na mimi nilikasirika kwa hiyo suala hilo tukalimaliza,” alisema.
Afukuzwe kazi. Period. Kumpiga mtu mzima sababu tu unacheo ni utovu wa nidhamu. Na kimbuzi ni nini. Alipe million moja akiomba radhi, na afukuzwe kazi iwe mfano wa kuheshimu watu. Hawa vijana hawafai kuwa viongozi hata.