28.2 C
Dar es Salaam
Friday, November 15, 2024

Contact us: [email protected]

DC awatahadharisha wavamizi wa mapori

Na MWANDISHI WETU-BIHARAMLO

MKUU wa Wilaya (DC) ya Biharamulo, Sada Malunde, amewataka wananchi wanaoendesha shughuli za kilimo na ufugaji katika Hifadhi ya Misitu ya  Biharamulo na Msitu wa Nyantakara wilayani humo, Mkoa wa Kagera, kuondoka katika maeneo hayo kabla hawajachukuliwa hatua.

Malunde alitoa agizo hilo juzi akiwa kwenye Msitu wa Nyantakara ambako alikuwa na Kamati ya Ulinzi na Usalama ya Wilaya ya Biharamlo pamoja na maofisa wa Wakala wa Misitu Tanzania (TFS).

“Msitu huu umevamiwa kwa kasi na kuharibiwa na watu wanaoendesha shughuli za kilimo na ufugaji kinyume cha sheria.

“Hali hii inatishia zaidi baada ya Serikali kupandisha hadhi Mapori Tengefu ya Kimisi, Burigi na Biharamulo kuwa Hifadhi za Taifa, ambapo kuna sheria zinazowabana wananchi kufanya shughuli za kibinadamu.

“Kwa hiyo, mimi kama kiongozi mwenye dhamana ya kusimamia utekelezaji wa sheria, sitakubali hali hii iendelee, nawataka muondoke kwa hiari na kwenda kuishi kwenye vijiji vinavyotambulika kisheria kabla Selikali haijatumia nguvu kuwaondoa.

“Pamoja na hayo, naona ni wakati mwafaka sasa kwa Serikali kuangalia uwezekano wa kurekebisha sheria za misitu na kuzifanya ziwe kali zaidi ili kuepuka uharibifu wa hifadhi za misitu nchini,” alisema Malunde.

Naye Mtendaji Mkuu wa TFS, Profesa Dos Santos Silayo, alisema vijiji vinavyoanzishwa katika maeneo ya misitu bila kufuata taratibu, vinaanzishwa kinyume cha sheria na kuahidi kushirikiana kikamilifu kudhibiti uvamizi na uharibifu wa misitu wilayani humo.

Kwa upande wake, Meneja wa TFS, Kanda ya Ziwa, Cosmas Ndakidemi, aliwataka wakazi wanaoishi maeneo ya jirani na Misitu ya Hifadhi ya Biharamulo na Msitu wa Nyantakara, kuheshimu mipaka na taratibu zilizopo ili wasiwajibishwe kisheria.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
591,000SubscribersSubscribe

Latest Articles