28.2 C
Dar es Salaam
Sunday, November 24, 2024

Contact us: [email protected]

DC ATAKA WAZAZI WA WANAFUNZI WAJAWAZITO WASEKWE RUMANDE

Na HARRIETH MANDARI  – GEITA


MKUU wa Wilaya ya Chato, Shaban Ntarambe, ametoa agizo kwa maofisa na watendaji wa kata zote wilayani humo  kuwasweka rumande wanafunzi watakaokutwa na ujauzito pamoja na wazazi wao na wale wanaokataa kuwataja wahusika wa ujauzito huo  kukomesha mimba za utotoni.

Alitoa agizo hilo kutokana na  kuibuka tabia ya baadhi wanafunzi wanaokutwa wajawazito kuwaficha waliowapa mimba kwa lengo la kupoteza ushahidi wanapofikishwa kwenye vyombo vya sheria kujibu tuhuma hizo.

Ilielezwa kuwa Halmashauri ya Wilaya ya Chato inakabiliwa na changamoto kubwa ya mimba kwa wananfunzi.

Kwa mujibu wa takwimu, tangu Julai  mwaka 2015 hadi Juni mwaka huu   wanafunzi 134 wa shule za sekondari walikatiza masomo  baada ya kubainika kuwa ni wajawazito, wakati kwa shule za msingi wananfunzi 29 walibainika ni wajawazito.

Ntarambe aliyasema hayo kwenye mkutano wa hadhara uliofanyika katika Kata ya Buseresere wilayani hapa na kuliagiza jeshi la polisi kushirikiana na serikali na jamii kutekeleza agizo hilo.

“Kuna tabia imeanza kujitokeza katika wilaya yetu ambako wale wanafunzi waliokutwa na ujauzito wamekuwa wakiwaficha wanaume waliowapa mimba ili wasikamamtwe.

“Sasa naagiza ikitokea tena kuanzia sasa mwanafunzi anamficha mtuhumiwa basi yeye na wazazi wake wote wataswekwa rumande hadi hapo watakapotoa ushirikiano  kukomesha tatizo hilo lililokithiri,”alisema.

Aliwataka wananchi kuhakikisha wanawapeleka watoto wao shule na pia kuwafuatilia kila wanaporudi nyumbani badala ya kuwaachia walimu wao hasa kwa watoto wa kike ambao wengi wao ni watoro.

Mkazi mmoja wa Kata ya Buseresere, Adelina Mugisha aliunga mkono adhabu hiyo ya awali na kuongeza kuwa itasaidia wazazi kushiriki kwa ukamilifu katika kuwalea mabinti zao kwa kuwajibika.

“Kwa kweli agizo hili la mkuu wa wilaya kwa upande wangu nimelipokea kwa mikono miwili na hata ingewezekana adhabu ingeongezwa zaidi.

“Hiyo ni kwa sababu kwa sasa tatizo hili limeshakuwa sugu hapa kwenye Kata yetu, mabinti wengi hukatiza masomo yao kutokana na ujauzito,” alisema.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
591,000SubscribersSubscribe

Latest Articles