20.2 C
Dar es Salaam
Wednesday, September 28, 2022

VYAMA VIFANYE KAMPENI ZA KISTAARABU UCHAGUZI BUYUNGU

Na PATRICIA KIMELEMETA


HIVI karibuni, Tume ya Taifa ya Uchaguzi (NEC) ilitangaza uchaguzi wa marudio katika kata 79 na majimbo mawili likiwamo la Buyungu baada ya aliyekuwa mbunge wake, Mwalimu Kasuku Bilago kufariki dunia Mei 26, mwaka huu katika Hospitali ya Taifa ya Muhimbili (MNH).

NEC ilitangaza kufanyika kwa uchaguzi huo Agosti 12, mwaka huu, huku ikivitaka vyama vya siasa kuteua majina ya wagombea ambao watawania majimbo hayo na kuyawasilisha kwenye ofisi za tume hiyo kama sheria ya uchaguzi inavyowataka.

Lakini pia tume hiyo ilivitaka vyama hivyo kuwasilisha majina ya wagombea wa udiwani kwenye kata 79 zinazotarajia kufanyika kwa uchaguzi huo nchi nzima ili yaweze kujulikana.

Kutokana na hali hiyo, baadhi ya vyama vya siasa tayari vimepitisha majina ya wagombea hao kwenye majimbo tajwa.

Kwa upande wa Chama Cha Mapinduzi (CCM), kimemteua Christopher Chiza kuwa mgombea wake wa Jimbo la Buyungu, huku Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema) kikimpitisha Elia Michael.

Chama cha Wananchi (CUF) upande unaomuunga mkono Katibu Mkuu wa chama hicho, Maalim Seif Sharif Hamad, kimeeleza bayana kuwa hakisimamishi mgombea kwenye uchaguzi huo kwa madai kuwa chama hicho kipo kwenye mgogoro wa uongozi.

Chama hicho kiliwataka Ukawa kusimamisha wagombea bora, imara, madhubuti ili waweze kuungwa mkono na wapiga kura, jambo ambalo linaweza kuwapa ushindi kwenye uchaguzi huo.

Kutokana na hali hiyo, NEC inapaswa kusimamia uchaguzi huo kwa kufuata taratibu za kisheria na kujiepusha na vitendo vya kuegemea upande wowote, hali ambayo inaweza kusababisha migogoro ya uchaguzi.

Lakini pia, NEC inapaswa kushirikiana na vyombo vya ulinzi na usalama ili kuhakikisha hali ya utulivu inakuwepo wakati wote kuanzia kampeni hadi siku ya uchaguzi, hali ambayo itawatia moyo wananchi kujitokeza kwa wingi ili waweze kupiga kura.

Pia NEC ina jukumu la kuziba mianya ya wizi wa kura na kutangaza mgombea atakayeshinda kihalali kwenye uchaguzi huo, jambo ambalo linaweza kuepusha migongano.

Ni matumaini yangu kwamba katika uchaguzi huu, NEC ikifuata taratibu zote za uchaguzi, hakutakuwa na malalamiko ya aina yoyote kutoka vyama vya siasa hasa upinzani kama ambavyo wamekuwa wakilalamika kila uchaguzi unapofanyika.

Vilevile, vyama vya siasa vinavyoshiriki uchaguzi huo navyo vinapaswa kufanya kampeni za kistaarabu ili kuepusha vurugu kama ambavyo ikitokea katika chaguzi zilizopita.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
202,097FollowersFollow
554,000SubscribersSubscribe

Latest Articles