Na ELIZABETH KILINDI – NJOMBE
MKUU wa Wilaya ya Wanging’ombe mkoani hapa, Ally Kassinge, amewaagiza walimu wakuu wa shule za msingi na sekondari wilayani humo kuwapima mimba wanafunzi wa kike baada ya kutoka likizo.
Agizo hilo alilitoa juzi alipozungumza na wananchi wa Mji wa Ilembula Wilaya ya Wanging’ombe.
Alisema imebainika mimba nyingi hupatikana watoto hao wakiwa likizo.
“Hivi sasa shule zimefunguliwa na wanafunzi wa kike wanaporudi hakikisheni mnawapima kujua kama wana mimba ili kujua kama wametoka nayo likizo na si shule. Hatua hiyo ikikamilika nileteeni ofisini kwangu ndani ya wiki mbili,” alisema Kassinge.
DC huyo alisema ni jukumu la mzazi kuhakikisha anampeleka mwanafunzi wake wa kike shuleni na kukaa shuleni kwenye mabweni na si kubaki nyumbani.
“Nilishaagiza wanafunzi wa kike wote hawatakiwi kukaa nyumbani kama shule ina mabweni, ni lazima wakae shuleni,” alisema.
Mbali na hayo, Kassinge alitoa wito kwa wadau wa elimu kuwekeza wilayani humo, kuharakisha suala zima la ukuaji wa elimu bora kwa faida ya vizazi vya sasa na baadaye.
“Niwaombe wadau wa elimu nchini kuwekeza zaidi katika wilaya yetu kuwapo upatikanaji wa elimu bora kwa vizazi vya sasa na vijavyo… wadau wa elimu wakijitokeza kuwekeza, hakika elimu itapatikana kwa urahisi na yenye ubora,” alisema Kassinge.