Na TUNU NASSOR-DAR ES SALAAM
SHIRIKA la Majisafi na Majitaka Dar es Salaam (Dawasco) limevunjwa rasmi na kuunganishwa katika Mamlaka ya Majisafi na Majitaka Dar es Salaam (Dawasa).
Akizungumza Dar es Salaam jana katika sherehe za kuunganishwa kwa Dawasa na Dawasco, Katibu Mkuu wa Wizara ya Maji na Umwagiliaji, Profesa Kitila Mkumbo, alisema kitendo cha kuunganishwa kitaokoa Sh bilioni 2.9 kila mwaka zilizokuwa zikipotea katika uendeshaji wa Dawasa na Dawasco.
Alisema fedha hizo zitakwenda kusaidia upatikanaji wa huduma ya maji katika Mkoa wa Dar es Salaam na Pwani.
“Serikali iliamua kuunganisha Dawasa na Dawasco ili kupunguza matumizi na fedha hizi zitaimarisha miundombinu na kuboresha huduma za maji katika eneo la huduma,” alisema.
Pia aliwaonya wafanyakazi wa Dawasa mpya kuacha tabia ya dharau, nyodo, kukumbatia matatizo na kuomba rushwa kwa wateja.
“Baadhi yenu mmekuwa na nyodo, rushwa na kuridhika na mafanikio kidogo, tabia hizi zikome kuanzia sasa,” alisema.
Aliitaka Dawasa mpya kujiendesha kama kampuni binafsi inayolipwa na wananchi wa Dar es Salaam na si idara ya Serikali ili kuongeza makusanyo ya fedha.
“Niwaombe mpunguze upotevu wa maji ambao kwa sasa asilimia 47 ya maji yanayozalishwa na Dawasa yanapotea,” alisema.
Kwa upande wake, Ofisa Mtendaji Mkuu wa Dawasa, Cyprian Luhemeja, aliahidi kukamilisha miradi mitatu na kutoa mwendelezo wa mingine ndani ya siku 100.
“Zawadi yetu kwa Magufuli hadi kufikia Desemba 9, mwaka huu ni kukamilisha mradi wa maji wa Chalinze, usambazaji wa maji upande wa Goba, Tegeta na maeneo mengine yaliyo karibu,” alisema.
Pia alisema ndani ya siku 100 watafunga mita nyingi za malipo ya kabla na wanaanza ujenzi wa matenki ya Pugu na kusanifu upya mradi wa visima vya Mpera.
“Ndani ya siku hizo pia tutaongeza mapato kutoka shilingi bilioni tisa hadi kufikia shilingi bilioni 12 na tutahakikisha tunapunguza upotevu wa maji,” alisema.