TUNU NASSOR, DAR ESSALAAM
MAMLAKA ya Majisafi na Majitaka Dar es Salaam (DAWASA) imeshtukia mchezo mchafu unaofanywa na watu wasio waaminifu wanaowataka wananchi kununua vifaa na kuchimba mitaro kuunganishiwa maji safi.
Akizungumza Dar es Salaam jana, Ofisa Mtendaji Mkuu wa Dawasa, Cyprian Luhemeja alisema kumekuwapo na malalamiko kutoka kwa wananchi kuombwa fedha za vifaa nakulazimishwa kuchimba mitaro jambo ambalo si sahihi.
Alisema kwasasa mamlaka hiyo ina vifaa na watumishi wa kutosha, hivyo wananchi wasikubali kuombwa fedha wala kuchimbishwa mitaro.
“Tuna watumishi wa kutosha kwa sasa na vifaavipo, hivyo wasidaganywe kutoa fedha za vifaa wala kuchimba mitaro ndipo wapate huduma ya maji,” alisema Luhemeja.
Alisema iwapo watatokea watu watakaolazimisha wananchi kuchimba mitaro na kuomba fedhaza vifaa, watoe taarifa kwa mamlaka hiyo ili waweze kuwachukulia hatua za kinidhamu haraka.
“Tuna huduma ya kuunganisha wateja kwa mkopo, hivyo kwa mwenye uhitaji wa maji afike katika ofisi za Serikali za mitaa ama Dawasa apate huduma hiyo na wala si kwa kupitia watu wengine,” alisema Luhemeja.
Kuhusu mafanikio ya siku 100 za uongozi wake, Luhemeja alisema jumla ya miradi saba yamaji imekamilika na imeanza kutoa huduma.