Na Mwandishi Wetu, Mtanzania Digital
KATIBU Tawala wa Wilaya ya Malinyi, Saida Mhanga amewataka Maofisa Maendele ya Jamii wa Kata, Watendaji wa Vijiji na Kata kusimamia Kanuni za Utawala Bora katika kutekeleza wa majukumu yao ya kila siku.
Akizungumza katika semina iliyoandaliwa na Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya Wilaya ya Malinyi, Khamis Katimba mwishoni mwa wiki, DAS Saida alisema, maofisa hao wanapaswa kutekeleza wajibu wao kwa maslahi ya wnaanchi.
“Kumekuwa na malalamiko mengi yanatoka kwa wananchi yanapelekwa Ofisi ya Mkuu wa Wilaya ambapo ukichunguza kwa makini, unaona ni kutotekelezwa kwa majukumu ya watendaji katika maeneo yao ambapo masuala hayo yangeweza kutatuliwa tangu mwanzo,,” alisema Saida Mhanga.
Aidha aliwataka watendaji hao kuandaa boksi la kupokea maoni/mapendekezo kutoka kwa wananchi, na kuongeza watendaji hao waendeshe vikao vya kisheria na wasome taarifa za mapato na matumizi ili wananchi wawe na imani na serikali yao.
Akitoa mada ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa, Kamanda wa TAKUKRU, Wilaya ya Malinyi, Sikujua Kimweri aliwataka watumishi kuzingatia miongozo na taratibu za kazi.
Kamanda huyo alisema kuwa, TAKUKURU ina lengo la kuhakikisha kuwa shughuli zote za serikali zinapangwa na kufanyika kwa mujibu wa taratibu ili wananchi waone kazi zinazofanywa na serikali yao.
Sikujua aliwataka watendaji hao kuhakikisha kuwa, mapato ya halmashauri yanakusanywa na yanatumika kwa usahihi kulingana na bajeti ilivyo.
Aliwataka watendaji hao kuwa makini na fedha za miradi ambazo zinaenda kutekeleza miradi katika maeneo yao, na kuongeza miradi hiyo itekelezwe kwa mujibu wa BOQ, miongozo na kanuni za serikali.
Aliwataka watendaji hao kuzingatia taratibu hizo kwasababu, wakienda kinyume watakutana na mkono wa sheria.
Mkuu wa Idara ya Kilimo, Mifugo na Uvuvi, Gipson Absalom aliwaambia watendaji kuwa, idara yake inafanya kazi kwa ukaribu na mamlaka ya hali ya hewa, na kwa mujibu wa utabiri wa hali ya hewa, Wilaya ya Malinyi itakua na mvua chache, za wastani na chini ya wastani.
Kutokana na vipimo hivyo, aliwataka watendaji washirikiane na maofisa kilimo waliopo katika kata na vijiji kutoa elimu kwa wananchi kuhakikisha wanapanda mazao yanayostahimili maji au mvua chache.
Na kwamba, wale wanaotaka kulima mpunga, wachague maeneo amabayo yanaweza kuwa na majimaji ya kutosha.