25.9 C
Dar es Salaam
Monday, November 25, 2024

Contact us: [email protected]

Dar ya Kijani yawasomba diwani, Katibu wa Mnyika

ASHA BANI-DAR ES SALAAM

KAMPENI ya Dar es Salaam ya Kijani inayoratibiwa na Umoja wa Vijana wa Chama Cha Mapinduzi (UVCCM), imewasomba Diwani wa Kata ya Kwembe, Dweza Horace Kolimba (Chadema) na Katibu wa Mbunge wa Kibamba,  John Mnyika, Liberata Samson kwa kujiunga na CCM.

Akiwapokea wanachama hao jana jijini Dar es Salaam, Naibu Waziri wa Kazi, Vijana na Ajira, ambaye pia ni Mbunge wa Dodoma Mjini,  Antony Mavunde, alisema mwaka 2020 ni lazima majimbo mawili la Ubungo na Kibamba yarudi CCM.

Mavunde alisema kuwa hiyo ni dalili tosha kwamba CCM watachukua majimbo hayo na ni aibu kuyaacha majimbo hayo mawili yakiwa upinzani.

Alisema kama makosa yalifanyika hapo awali hategemei  kurudiwa tena na majimbo hayo yakaachwa chini ya John Mnyika (Kibamba ) na Saed Kubenea (Ubungo), kwa kuwa hakuna wanachokifanya zaidi ya utekelezaji wa ilani ya CCM.

“Kama kuna uhitaji wa maji, barabara nzuri vyote vinafanyika sasa kuna haja gani ya kubakia upande wa pili wa upinzani ni lazima vijana kufanya kazi kuhakikisha majimbo yanarudi CCM na katika uchaguzi wa serikali za mitaa kata zote ziwe chini ya chama hicho.

“Jitahidi hapa viongozi hii ni aibu anzeni na mitaa yote 91 kuhakikisha inarudi CCM maana hapa nikiangalia hakuna hata pa kupita Mnyika wala Kubenea watapitia wapi?

“Jukumu la chama cha siasa ni ushindi na kushika dola na ili ushinde ni lazima kuishi matatizo ya wanajamii sasa kwa serikali ya sasa imefanikiwa kwa kiwango kikubwa kutatua changamoto za wananchi wake,” alisema.

Hata hivyo alisisitiza kuwa Rais Dk. John Magufuli anakubalika ndani na nje ya nchi huku akitolea mfano, alipokuwa Afrika Kusini juzi wakati wa kuapishwa Rais Cyril Ramaphosa, alishangiliwa na wananchi wa Afrika Kusini.

Katika hatua nyingine Mavunde aliwataka vijana kufanya kazi kwa bidii, kujiajiri wakati wakisubiri mchakato wa Serikali katika kuongeza ajira kwa vijana hao.

Aliwataka kuhakikisha wanakuwa katika vikundi vya ujasiriamali vya kukopeshana ili waweze kupata fedha kwani Ubungo ina fedha nyingi ambazo zimetengwa kwa ajili yao waweze kukopeshwa na kujiendeleza.

Katika hatua nyingine aliwapongeza Mkoa wa Dar es Salaam kwa kuanzisha kampeni ya Dar ya Kijani kwa kupandisha bendera ya CCM kila kata.

Kwa upande wake Mwenyekiti wa UVCCM Mkoa wa Dar es Salaam, Mussa Kilakala,  alisema wanashirikiana vizuri na viongozi wa majimbo ya Ubungo lakini bado watahakikisha kata zote 14 na majimbo ya Wilaya ya Ubungo zinarejea CCM kwani ziliazimishwa kwa muda.

“Jimbo la Ubungo na Kibamba lazima yachukuliwe na CCM mwaka 2020, hakuna sababu ya kubaki upinzani kwani Rais Magufuli anafanya mambo makubwa ndani ya CCM na Taifa kwa ujumla.

“Na hii kampeni ya Dar ya Kijani itaambatana na kazi ya kutundika bendera, ufunguzi wa matawi kwa kila kata za Mkoa wa Dar es Salaam kuelekea Uchaguzi wa Serikali za Mitaa pamoja na Uchaguzi Mkuu mwaka 2020. Hivyo ni jukumu letu vijana kujipanga na kuhakikisha tunarejesha heshima ya chama chetu CCM,” alisema Kilakala.

Waliohama chama wanena

Kolimba na Liberata waliushukuru uongozi wa ubungo kwa kuwapokea na kuahidi kuwa watafanya kazi kuhakikisha chama hicho kinachukua kata hizo walizotoka.

Kolimba alisema alikuwa katika chama chenye vurugu na kisichokuwa na mikakati ya maendeleo huku akisema anaogopa kuendelea kubaki katika  chama ambacho kila kukicha ni vurugu.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
591,000SubscribersSubscribe

Latest Articles