25.4 C
Dar es Salaam
Saturday, November 16, 2024

Contact us: [email protected]

DAR MCHANA IMEDORORA, USIKU IMESINZIA

Kina Mama wakifanya biashara maeneo yasiyo rasmi

Na Dennis Luambano, Dar es Salaam

NIMEWAHI kuandika siku za nyuma kuhusu Dar es Salaam kuwa ni jiji maarufu, pia ni mji mkuu wa kibiashara hapa nchini.

Hilo halina ubishi, leo narudia kuandika kuhusu Dar es Salaam kutokana na ukweli kwamba mabadiliko yake yanakwenda kwa mwendo wa kinyonga, licha ya tenzi mbalimbali kughaniwa kuwa kuna Dar es Salaam mpya itazaliwa. 

Dar es Salaam ni jiji la kodi, kwa maana makusanyo yake ni makubwa kuliko mikoa mingine yote iliyopo Bara na Zanzibar.

Kwamba inasemekana asilimia 80 ya mapato yanayokusanywa na Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) yanatoka Dar es Salaam na si sehemu nyingine.

Kimsingi, haikuwa bahati mbaya kwa Dar es Salaam kuwa ilivyo leo, bali historia yake inasema ilichaguliwa na wakoloni (Wajerumani) kuwa mji mkuu wa Afrika ya Mashariki kwa sababu ya bandari asilia yenye mdomo mpana wa Mto Kurasini.

Historia hiyo inaeleza zaidi kuwa, kuanzia mwaka 1891 ilichukua nafasi ya Bagamoyo kama makao makuu ya utawala.

Bandari pamoja na ujenzi wa reli ya kati kwenda Kigoma tangu mwaka 1904 ziliimarisha nafasi ya mji ulioendelea.

Katika Bahari ya Hindi ni bandari kubwa nchini Tanzania inayojihusisha na usafirishaji na uingizaji wa bidhaa mbalimbali za kilimo, ufugaji, ujenzi, magari na dawa.

Pamoja na neno Dar es Salaam kumaanisha nyumba ya amani kwa lugha ya Kiarabu, lakini katika siku za hivi karibuni jiji hilo limekuwa kero, hasa katika maeneo ya katikati ya jiji.

Limekuwa kero kutokana na foleni ya magari, hasa katika muda wa asubuhi na jioni, licha ya Mradi wa Mabasi yaendayo Haraka (UDART) kuanza kazi. Kwa muda mrefu sasa kero hii imekosa suluhisho.

Wanaopaswa kuitatua wanashauri watu wawe wanadamka asubuhi na mapema kwa ajili ya kuiepuka. Unajua kwanini wanatoa ushauri huo? Kimsingi, akili zao zimefika omega katika kufikiri na wanadhani kero hiyo ni ya asili, kwa hiyo haiepukiki, kisa kuna ofisi kuu za viongozi wa Serikali, mabalozi na mashirika ya kimataifa.

Wamekosa ubunifu na mawazo mbadala, kwa hiyo wanahalalisha ushauri wao kuwa mtu anayeishi Bunju anatakiwa kuamka saa 11 alfajiri ili awahi kufika eneo la Posta lililopo katikati ya Jiji la Dar es Salaam.

Mtu huyo hana tofauti na abiria anayetoka Dar es Salaam kwenda Mbeya, anayetakiwa kudamka alfajiri ili awahi usafiri katika Kituo cha Mabasi cha Ubungo.

Kutokana na foleni kuwa kero ya asili, ndiyo maana Dar es Salaam imedorora kwa sababu watu wanatumia muda mrefu barabarani wakati wa kwenda katika shughuli zao, pia wanatumia muda mrefu kurudi nyumbani kwao.

Mbali na kero ya foleni, kuna kitu kingine cha ajabu cha akina mama kuuza vitumbua, chapati na maandazi muda wa asubuhi katika Kituo cha Mabasi cha Posta Mpya. Kwa muda mrefu sasa kina mama hao wanauza vitafunwa hivyo bila kujali kanuni za afya, kwa maana vinauzwa bila kufunikwa. Walianza kuuza vitafunwa hivyo hata kabla ya Rais Dk. John Magufuli hajatoa tamko la kuwataka viongozi wa mikoa nchi nzima kutowabughudhi wamachinga hadi pale watakapotengewa maeneo rasmi ya kufanyia biashara zao. Ndiyo, kabla Magufuli hajatoa agizo hilo mwanzoni mwa Desemba, mwaka jana, kina mama hao waliendelea na biashara hiyo na askari mgambo wa jiji walishindwa kuwachukulia hatua kwa kuwa waliwaomba rushwa.

Swali la kujiuliza hapa, iweje eneo la Posta Mpya ambalo ni kama sebule ya Dar es Salaam kuwe na msururu wa kina mama wakiwa wamepanga ndoo zao zenye chapati na maandazi?

Mbali na suala la kina mama kuuza vitafunwa, pia usiku ikifika Dar es Salaam nayo inasinzia, kwa sababu ni moja kati ya jiji ambalo giza likiingia shughuli zote za kusukuma na kukuza uchumi zinasimama.

Ndiyo, haiwezekani jiji ambalo TRA inakusanya karibu asilimia 80 ya mapato yake lizizime pindi giza linapoingia.

Hakika hatuwezi kusonga mbele kama tunavyotaka ikiwa eneo pekee ambalo ni kitovu kikuu cha uchumi hakuna shughuli zinazofanyika kwa muda wa saa 24.

Hali hii ni tofauti na majiji mengine ambako kwa muda wa saa 24 katika siku saba za wiki kuna shughuli mbalimbali za kiuchumi zinafanyika. Watu hawalali, bali wanabadilishana muda wa kuingia tu, lakini kazi zinaendelea kufanyika kama kawaida na matokeo yake yanaonekana. Kimsingi, hali hiyo ni tofauti na katikati ya Dar es Salaam ambako giza likiingia migahawa inafungwa, magari ya kusafirisha abiria yanapungua na ofisi zote zinafungwa.

Nini kifanyike kuhakikisha Dar es Salaam haidorori mchana wala haisinzii usiku? Binafsi, sina jibu la moja kwa moja, ila naamini kuna watu waliobobea katika masuala hayo ambayo naamini waliwahi, wamewahi na wataendelea kutoa suluhisho la kufanya ili Dar es Salaam isonge mbele.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
591,000SubscribersSubscribe

Latest Articles